Zinazobamba

VETA YAJIPANGA KUONGEZA UDAHILI




MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Fundi Stadi (VETA), imesema kuwa imejipanga kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 740,000 hadi kufikia 1,000,000 ifikapo 2021/22.

Pia VETA imewaalika wananchi kutembelea banda lao lililopo katika viwanja vya maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam 'Sabasaba', ili kujionea teknolojia mbalimbali.

Hayo yameelezwa na Meneja Uhusiano wa Mamlaka hiyo, Sitta Peter alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika banda lao lililopo katika viwanja vya maonesho hayo. 

Amesema VETA imejipanga kuwajengea uwezo vijana wawe na ubunifu wenye umahiri wa kubuni vitu mbalimbali kwa mahitaji ya jamii.

"Hii yote tunaonesha ni kwa namna gani tunachangia katika sekta ya viwanda, kwa mfano kwa mwaka huu wa fedha ulioisha kulikuwa na miradi 40 ya ujenzi na upanuzi wa vyuo. Katika hiyo miradi inahusisha pia vyuo vipya 25 vya Wilaya ambavyo tunavijenga kwa nguvu za ndani," amesema. 

Ameongeza kuwa, pamoja na miradi hiyo, pia wana miradi mingine 10 ya Halmashauri na hivi karibuni wamezindua vyuo vitatu katika Halmashauri ya Ileje, Nkasi na Nyamidaho.

Akizungumzia kuhusu maonesho hayo, amesema kuwa kwa mwaka huu wamefanikiwa kuja na teknolojia 12 mpya zikiwamo mashine ya ubuyu, kuchemsha maji pasipo kutumia umeme, mfumo wa kunawa maji bila koki, kuingiza umeme mita ukiwa mbali, ushonaji wa kidigitali, mashine ya kupanda mazao, ukaushaji bora mazao ya Samaki na nishati ya umeme pasipo chanzo cha mafuta wala maji. 

Pia teknolojia nyingine ni teknolojia ya kuchenjua madini kutoka kwenye madini pasipo kutumia zebaki, ubunifu wa samaki kikiwamo kitanda tiba na kochi.

Hakuna maoni