Watanzania msaidieni Manyinyi, huu mwaka wa nane bado anateseka na maradhi
Na Selemani Magali na Bint Ally Ahmed
Kijana Ali Sunyami Manyinyi, mzaliwa wa Bunda Mjini mkoani Mara, anaumwa sana.
Manyinyi ni fundi bobezi wa magari (Mechanics) katika kutengeneza injector pump za magari kwenye gereji moja iliyopo Mgomeni jijini Dar es Salaam.
Janga lilimkuta mwaka 2012 wakati alipokuwa anafanyia matengenezo gari la mteja wake huko Visiga, Kibaha kufuatia gari hiyo kupata hitilafu eneo hilo na alihitajika kulifanyia matengenezo.
Awali walikuja watu ofisi Magomeni na kumweleza kuwa gari lao limepata hitilafu, wakadai kuwa kifaa mwendo cha gari yao (gear box) imepasuka huko Visiga, Kibaha mkoani Pwani.
“Kilichonishangaza ni kwamba gari ikiwa imesimama ‘Gear box’ haiwezi kupasuka, hiyo ingekuwa ni mara ya kwanza kutokea na kushuhudia”.
Alitoka ofisini na kwenda huko Visiga kukagua ubovu wa gari hiyo.
“Nakumbuka ilikuwa wakati wa jioni hivi, nilitoka ofisini na kwenda kuangalia gari hilo, bahati nzuri nilipofika na kuliangalia, nikagundua injector pump yake ina shida, nikaifungua nikarudi nayo ofisini Magomeni, tukaitengeneza kisha nikarudi kwenda kuifunga tena kule Visiga.
“Injector pump ile ilikuwa na pande mbili, upande mmoja inatumia umeme, upande mwingine ‘mechanical’ ya kawaida, sasa ilionekana upande wa umeme ndio ulikuwa na shida kwa hiyo tulikitoa kipande cha umeme na kubakisha upande wa ‘mechanical’, lengo ni kuifanya iwake. Alieleza Bw. Manyinyi.
Wakati anapiga ‘resi’ (anakandamiza pedeli ya mafuta) kwa kutumia mkono huku akichunguza tatizo la gari la mteja wake, haikufahamika mara moja kilitokea kitu gani, alijikuta animepigwa na kitu kizito tumboni na mkononi na kuhisi maumivu makali sana, alikimbizwa hospitali ya Tumbi, Kibaha na hapo alipofanyiwa uchunguzi na kubainika kuwa amepata matatizo makubwa tumboni na sehemu zake za siri, sehemu zote zikihitaji upasuaji.
Kesho yake alfajiri alipelekwa hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na matibabu zaidi baada ya madaktari wa Hospitali ya Tumbi kuona tatizo ni kubwa zaidi.
Anasema bahati nzuri ni kwamba alifanyiwa upasuaji wa tumbo siku ile ile alipofikishwa Muhimbili na zoezi lilifanikiwa akapona, maumivu yote yalikwisha. Tatizo likabaki kwenye sehemu yake ya haja ndogo.
Hali hiyo imelazimu madaktari kumsaidia kwa kumwekea mpira maalum wa haja ndogo, ili aendelee kupata haja hiyo huku akisubiri matibabu zaidi na maajaliwa ya mwenyezi mungu.
Madaktari walimwambia asubiri upasuaji wa njia ya mkojo na atafanyiwa baadae. Alisubiri hadi ilipofika Novemba, 2013, akapewa barua aende Hospitali ya KCMC Moshi, na wakati huo kulikuwa na wataalam wa kizungu waliokuja kutoa matibabu hospitalini hapo.
Bahati mbaya barua alipewa kwa kuchelewa na alipofika Moshi alikuta ratiba ya watu wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji ilishatoka na yeye sio miongoni mwao.
Hakuwa na namna, ilimbidi afunge safari ya kurudi Muhimbili tena, alivyofika akapata tatizo jingine. Watu wa Muhimbili walimwambia kuwa tayari alisharuhusiwa, hivyo akitaka arudi anatakiwa aanze upya. Alijiuliza sana kwa nini hivyo wakati yeye bado anahitaji huduma na hajapona.
Manyinyi anabainisha kuwa wakati akiwa bado anajishauri nini cha kufanya, bahati nzuri akakutana na daktari mmoja ambaye anamfahamu, akamueleza shida inayomkabili.
Daktari huyo akamwambia kuwa yeye hataweza kumsaidia, lakini anaweza kumkutanisha na daktari ambaye atamsaidia, alimshukuru sana maana aliona sasa kuna tumaini jipya.
Hatimaye alikutanishwa na Daktari Prof. Yongoro, ambaye alieleza kuwa ndiye anayemiliki hospitali ya Upanga inayofanya upasuaji wa magonjwa kama yake.
Ilikuwa mwaka 2014 alipokutana naye rasmi, lakini alivyodhani ikawa tofauti. Daktari alisema gharama za hospitalini kwake zilikuwa ni ghali sana ukilinganisha na za Muhimbili, alimshauri arudi tena Muhimbili, naye atamsaidia kumfanyia upasuaji.
Alirudi Muhimbili siku ambayo aliahidiwa, akakutana nae na alipoulizia ratiba za pale Muhimbili, ikaonekana hakuna nafasi ya kufanyiwa upasuaji. Alimpangia kurudi tena baada ya miezi sita.
Ikumbukwe kuwa hiyo ilikuwa ni Juni 2014, alitakiwa arudi Desemba 2014. Manyinyi hakuchoka, alikubaliana na ratiba hiyo.
Ilipofika Desemba 8, 2014 dana dana iliendelea, alipofika Muhimbili aliambiwa baadhi ya madaktari wamekwenda likizo kwa hiyo hilo suala lake likashindika.
Akapangiwa tena tarehe ya kurudi baada ya wiki mbili, nayo ilipofika pia ikawa tatizo ni lile lile.
Akakutana na daktari mwingine kabisa, naye akampa tarehe ya mbali sana, akamwambia kuwa kwa ratiba zilivyo, anahitajika kwenda tena hospitalini hapo Septemba 14, 2015, yaani akae nyumbani miezi tisa bila ya matibabu.
Kabla Manyinyi hajaanza kuinua nyayo zake na kuondoka, akakutana na daktari mwingine ambaye anamfahamu kidogo, akamueleza hali ilivyo, alisikitika na kumuuliza nani aliyempangia muda huo?
Akamweleza na baada ya hapo hakujua kimefanyika nini, tarehe ile ikabadilishwa na kupangiwa Januari 19, 2015, ahudhurie hospitalini.
Tarehe hiyo ilipofika akalazwa tayari kwa kusubiri upasuaji, Bw. Manyinyi akaona sasa tatizo lake linaenda kupatiwa ufumbuzi. Haikuwa hivyo, ilipofika siku ya upasuaji, walikuwa watu watatu ambao wanatakiwa kufanyiwa huduma hiyo, yeye alipangwa mtu wa tatu, wenzake wawili walibahatika kufanyiwa ila yeye hakubahatika.
Baada ya mizunguko mingi sana, alikuja kubahatika kufanyiwa upasuaji, hata hivyo upasuaji wenyewe haukufanikiwa, tatizo likawa bado linamsumbua, akashauriwa aende India kwa matibabu zaidi.
Baada ya hapo alianza kufanya mazungumzo na hospitali tatu nchini India na zote walimpa gharama zake mpaka kupona kabisa na kurudi kufanya shughuli zake kama zamani.
Anatakiwa kutoa kiasi cha dola za Kimarekani Elfu kumi ($10,000) sawa na fedha za Kitanzania shiling milioni 24,000,000.
Hizi ni gharama za nauli ya kwenda na kurudi, malazi nchini India na matibabu.
Aliambiwa kwa tatizo lake atalazwa hospitali kwa siku nne, lakini atatakiwa kukaa India kwa muda wa mwezi mmoja kutizamwa zaidi kabla ya kupanda ndege kurudi nyumbani.
Kutokana na shida hiyo inayomkabili, Bw. Manyinyi anawaomba msaada watanzania wenzake watakaoguswa na anayopitia sasa.
Kwa kweli anateseka sana na matibabu ndio kama hivyo hajapata, maisha yake yamekuwa ni mtihani, hapati haja kwa njia ya kawaida, anatumia mipira na kila baada ya muda ni lazima abadilishe, maisha yake yamekuwa hivyo kwa miaka nane sasa.
“Jamani ndugu zangu naombeni msaada wenu, kwa kweli napitia wakati mgumu.
Zamani nilikuwa na mwenzangu ambaye nilipanga kuishi naye na kujenga familia yetu pamoja, lakini kwa mtihani huu, mwenzangu ameamua kwenda kufunga ndoa na mtu mwingine… (akilia kwa uchungu), nisaidieni watanzania”. Alieleza Bw. Manyinyi kwa uchungu.
Kwa kweli nilimuona wakati nazungumza naye, maisha yake ya sasa yamejaa huzuni, anaonekana kujitahidi sana kukabiliana na hali aliyo nayo lakini sasa.
“Hata hivyo bado namuomba Mungu kisha najipa moyo kwamba, Mungu atawainua watu watakuja kunisaidia na tatizo hili litakwisha”. Anasema kwa tumaini Bw. Manyinyi.
Anasema tatizo hili kwake ni kubwa lakini kwa Allah ni dogo sana, anaweza akabadilisha maisha yangu muda wowote, yuko mbele yenu, yeyote atakayesoma makala hii ajue kuwa ndugu yake anateseka, anaomba kila mwenye chochote amchangie, na kwa mwenye uwezo wa kumpeleka India atashukuru zaidi.
Mnaweza kutuma msaada wenu kupitia namba ya Ukht. Mariam Said 0713 300 024, ambaye ndiye msimamizi mkuu wa suala lake la matibabu, au namba ya mkononi ya mgonjwa, 0719 41 55 11 jina litatokea James Sunyami Manyinyi, au nambari 0712 45 42 72 Nuru Hamza Olaiti, ambaye ndiye mlezi wake na msimamizi wa suala hili.
Lakini pia unaweza kupitisha michango yako kupitia benki ya Amana akaunti namba 005141620660001, jina la Akaunti ni Wanawake Wema Foundation.
Bw. Manyinyi alimaliza elimu yake ya msingi katika shule ya Terita iliyopo kijiji cha Mwibage, Bunda mkoani Mara.
Safari yake ya kuja Dar salaam kutafuta maisha ilianza mwaka 2004, dhamira ikiwa ni kujiendeleza na masomo.
Hata hivyo alipofika jijini hakuweza kufanikiwa lengo lake, alijikuta anaishia kufanya biashara ndogo ndogo.
Alianza kuuza mifuko ya plasiki maarufu wakati huo kama ‘rambo’ katika masoko.
Baadae akajishughulisha na kuuza nguo mitaani.
Alifanya shughuli hiyo hadi alipopata fursa ya kujiunga na gereji iliyopo Magomeni Mapipa. Kazi hii ilikuwa inakwenda vizuri hadi shida aliyo nayo inamkuta.
ALI SUNYAMI MANYINYI NA WANAWAKE WEMA FOUNDATION
Ilikuwaje akakutana na Jumuiya ya Wanawake Wema foundation?
Ali Manyinyi anasema ni Mungu tu! “Shemeji yangu ni mtu ambaye ameishika dini, sasa alibahatika kuungwa katika group la waumini wenzake, huko akakutana na kundi hili la Wanawake Wema, akaangalia faida ambazo zinapatikana mle akagundua kuwa ni kundi lenye faida maana mara nyingi wanashughulika na kusaidia yatima na wajane, akaona ni jukwaa zuri la kueleza changamoto zake.
Hapo akamfuata mmoja wa viongozi wa kundi hilo (Admin) Ukht. Mariyam Saidi na kumtumia ujumbe wa moja kwa moja (Direct message), wakazungumza sana na hapo ndio ikawa mwanzo wa mimi kuanza kufahamika.
Anasema kuwa kiongozi wa kundi hilo alimuelekeza hatua za kufanya, ikiwemo kuwaambia watanzania juu ya tatizo lenyewe na waweze kumsaidia.
Kweli walifuata maelekezo yake, leo wametembelea baadhi ya vyombo vya habari kujieleza ili watu wajue namna anavyoteseka na kuomba usaidizi.
Ndoto za Manyinyi kabla ya kupatwa na tatizo hili, alitamani kufungua ofisi yake mwenyewe ya gereji, lakini kwa sababu ya maradhi aliyo nayo anaona hataweza kukamilisha, maisha yake ni kama yameingiwa na doa kubwa ambalo haliwezi kufutika.
Moja wa Kiongozi katika Kundi la Wanawake Wema Foundation, Ukht. Mariyam Saidi, amesema kuwa wao kama wanawake wamefanya juhudi kubwa sana ili kumpatia matibabu Manyinyi ili arudi katika hali yake ya kawaida.
Anasema kuwa mpaka sasa wamejichangisha na kupatikana kiasi cha cha milioni 1,800,000/, pesa zinazohitajika ni milioni 24,000,000/.
Amewaomba Waislam kushirikiana nao kwa hali na mali, ili kumsaidia kijana huyo aweze kuwa kama mwanadamu mwingine.
Ukht. Mariam amesema kuwa kundi la Wanawake Wema ni kundi linalojishughulisha na kuwasaidia yatima, wajane na wale wasiojiweza hivyo wanawaomba Waislam kuwaunga mkono.
No comments
Post a Comment