Ukarimu, upendo wa mama mwenye nyumba ulivyomsukuma Ester Mahindeka kusilimu
Na Mwandishi wetu
![]() |
Ester Mahindeka kusilimu |
Katika safu ya aliyesilimu wiki hii tunakuletea mahojiano na Ester Julius Mahindeka, msichana mwenye umri wa miaka 23, mkazi wa Dar es Salaam akielezea safari yake ya maisha hadi anaingia katika Uislamu.
Ester aliyesilimishwa na Imamu Msaidizi wa Kichangani, Sheikh Mursalina Mavere, sasa anajulikana kwa jina jipya la Kiislamu la Salha.
Fullhabari: Tueleze kwa ufupi historia yako
Ester: Mimi nilikuwa Msabato na nilibatizwa Kijichi, Mbagala Dar es Salaam. Wazazi wangu walifariki nikiwa mdogo: baba mwaka 2005 na mama mwaka 2007 na kuniacha na mdogo wangu anayeishi Tanga.
Baada ya wazazi kufariki, babu alinilea, akanisomesha hadi nilipomaliza darasa la saba, kisha nikajiunga na sekondari lakini alikatisha usimamizi wake kwangu nikiwa kidato cha pili. Hivyo, niliishia hapo kimasomo na kuanza safari ya kujitegemea. Nikaja Dar es Salaam na kuajiriwa kufanya kazi za ndani kule Buza, kisha nikapata mchumba akanioa.
Fullhabari: Nini kimekusukuma kuingia katika Uislamu?
Ester: Ni ukarimu wa Waislamu niliouona baada ya Mwenyezi Mungu kunipitisha katika mtihani mgumu. Ni kwamba, baada ya kuolewa, miezi sita baadae mume wangu alibadilika, akanikimbia na kuniachia chumba na madeni juu. Kitendo kile kilinivuruga sana kwa sababu nilimtegemea sana, hususan kimaisha.
Ninachoshukuru ni kwamba, mama mwenye nyumba, ambaye ni Muislamu, alinionea huruma sana, akanifariji na kuniambia nisikate tamaa kwani mimi bado ni kijana mdogo na naweza kuendelea na maisha yangu. Ulikuwa ni upendo wa hali ya juu.
Nikajiona kumbe ninao ndugu na sina sababu ya kukata tamaa. Sikujua kuwa, siku moja watu ambao nilikuwa nawaona ni wa hatari watakuwa ndio wasamalia wema na nguzo kwangu. Nilipoona upendo wa mama mwenye nyumba, nilijua haukuja hivihivi bali aliongozwa na imani yake. Hapo nikaona Uislamu ni dini ya upendo.
Wakati huo, sikuwa na msaada wowote kutoka kwa ndugu zangu wa damu, licha ya kuwaambia nimekimbiwa na mume. Kiufupi, baada ya wazazi wangu kufa, uhusiano wao na mimi pia ukafa. Hata kanisani nilikobatizwa, niliwaambia shida zangu lakini hakuna aliyenisaidia. Nilipita makanisa mengi kuomba msaada ili nianzishe biashara lakini ilishindikana.
Mdogo wangu pia ana mchango katika kusilimu kwangu. Yeye alitangulia kusilimu na akawa ananilingania nisilimu akitaja neema ambazo Mwenyezi Mungu alimbariki baada ya kusilimu. Huyu mdogo wangu aliyezaliwa mwaka 1999 ndio yule aliyopo Tanga na sasa anafanya kazi na ndugu zake wa Kiislamu ya kuuza nguo katika duka
.
Kabla kuamua kusilimu, mama alinifundisha Uislamu, hususan maadili na akanipeleka katika madrasa ya Sheikh Chizenga kujifunza zaidi, ikiwemo sala. Taratibu, nikaona naanza kubadilika kitabia, mathalan nikaanza kuvaa nguo ndefu
.
Haikuwa kazi rahisi lakini kwa sababu nilikuwa na dhamira ya kubadilika hatimaye nilizoea. Kwa sasa, kama unavyoniona naweza kuvaa hijabu na niqab vizuri, najua faida za kujistri… mafundisho kama haya sikuwahi kuyapata popote pale katika makuzi yangu.
Fullhabari: Umejiandaaje kwa namna watu watakavyokuchukulia baada ya kusilimu kwako?
Ester: Najua maisha yangu yatakuwa magumu. Kusilimu kutapelekea nitengwe na ndugu, jamaa na marafiki zangu wa awali lakini hiyo hainsumbui kwa sababu nimeamua kwa moyo wangu wote. Nikiwa kama msafiri hapa duniani, siwezi kuogopa macho ya watu halafu niache kumfuata Mungu wa kweli.
Nimeamua kuingia katika Uislamu nikiwa na akili zangu timamu na naamini Mwenyezi Mungu wangu atanisimamia na kunipatia marafiki wengine ambao watakuwa sababu ya mimi kuingia peponi. Nataka hapo kesho au kesho kutwa nitakaporejea kwa Mola niwa na majibu sahihi kwa kila kitu ambacho nimefanya katika uso wa dunia.
Fullhabari: Je mumeo alirudi na kukwambia kwa nini alikukimbia?
Ester: Mpaka sasa sijajua kilimkuta nini mpaka akanikimbia, lakini sitaki hata kukumbuka huko maana niliteseka sana kimawazo.
Nashukuru tu kuwa, kuondoka kwake kulinipatia mama mwingine aliyenionesha ukarimu hadi nikaupenda Uislamu. Mimi nilikuwa sifanyi kazi yeyote kwa hiyo kula na afya yangu vilimtegemea mama. Hata vazi hili unaloliona nimepewa na mama huyu ambaye kwangu namuona kama mkombozi.
Fullhabari: Ni nini matumaini yako kwa Waislamu?
Ester: Mimi nategemea Waislamu watanipokea na kunifundisha dini vizuri. Mama alinionyesha njia. Naamini Waislamu wengine watanifundisha zaidi ili baadae, Mungu akipenda, nijenge familia katika maadili yanayoridhiwa na Mwenyezi Mungu.
Fullhabari: Una mpango gani wa kutafuta shughuli ya kukupatia kipato?
Ester: Kaka yangu, mimi napenda sana kufanya kazi nijitegemee mwenyewe kwani nilipitia changamoto kwa sababu sikuwa na shughuli ya kujipatia kipato. Nikipata ajira kwa wasamalia wema, nitaifanya kazi hiyo kwa moyo wangu wote. Hata nisipopata ajira, niko tayari kufanya biashara, nikipata mtaji. Nawaomba Waislamu wanisaidie katika hilo.
Hata hivyo, napata moyo kwa sababu mama aliniambia, kama umeamua kuifia dini, Mwenyezi Mungu atakuinua, utapata ndoa nyingine na atakufikisha pale unapotaka. Alinishauri niwekeze imani yangu kwa Mwenyezi Mungu, naye ataitika dua zangu.
Na mimi nayakabidhi maisha yangu kwa Mwenyezi Mungu, nataka niwe mtu wa dini mwenye heshima ya Kiislamu ili hata wale waliokuwa wananitenga na kunitupa waone kuwa Mwenyezi Mungu bado yupo pamoja na mimi.
Fullhabari: Una wito gani kwa Waiislamu?
Ester: Waislamu wajue kuwa wamepata thamani kubwa kwa wao kuwa katika Uislamu, hivyo wasichezee nafasi hii. Jambo la muhimu tushirikiane tujaliane na kukirimiana.
No comments
Post a Comment