Zinazobamba

Sheikh Ponda: Uislamu unakabiliwa na vitisho ndani, nje ya nchi



Na Mwandishi wetu

Sheikh Ponda Issa Ponda, si jina geni katika masikio ya Watanzania, anafahamika sana katika juhudi zake za kuupigania Uislamu na pia kwa kuwa kwake mstari wa mbele  katika matukio mbalimbali ya harakati za Kiislamu. Mwandishi wetu,  alikutana na Sheikh Ponda hivi karibuni na kuzungumza naye kuhusu mambo kadhaa wa kadhaa ya maendeleo ya Uislamu na Waislamu. 


Fullhabari: Wasomaji wetu wangependa kujua historia yako kwa uchache. 

Sheikh Ponda: Mimi nisingependa kuelezea historia na wasifu wangu kwa sababu siamini kuwa hiyo ina faida katika jamii. Ninachoweza kufanya ni kuileza jamii kuwa Sheikh Ponda yupo hai na bado anaendelea na harakati zake za kutetea Waislamu na Uislamu. Pia, nimekuwa nikielimisha umma juu ya umuhimu wa kujikinga dhidi virusi vya corona.

Niseme tu, mimi nipo na nimekuwa ninakutana na waandishi wa habari mara kwa mara, hiyo inaonesha kuwa bado nipo, na  ndiyo maana hata wewe umekuja kupata habari kwangu ili kuwapasha Watanzania.


Fullhabari: Unaonaje utendaji wa taasisi za Kiislamu hivi sasa ukilinganisha na zamani?

Sheikh Ponda: Kwa ujumla utendaji wa taasisi za Kiislamu hapa nchini unaridhisha. Itakumbukwa kwamba, kabla ya kuzaliwa kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) tulikuwa na taasisi moja ya Afrika Mashariki East Africa Muslim Welfare Society (EAMWS) iliyokuwa na nguvu, iliyoheshimika na kukubalika. Hata hivyo,  kwa bahati mbaya EAMWS ilivunjwa na serikali, na ikaundwa BAKWATA. 

Matokeo yake, Waislamu walianzisha harakati za kudai haki ya kuanzisha taasisi zao huru. Haikuwa rahisi, lakini baada ya mvutano kidogo serikali iliridhia na taasisi zingine zilianza kusajiliwa. Mpaka leo hii tunapozungumza zipo taasisi nyingi ambazo zinafanya vizuri katika kusukuma maendeleo ya Waislamu na Uislamu ikiwemo The Islamic Foundation (TIF), Alhikma, DhiNurein, na Islamic propagation Centre (IPC), nk ambao baadhi wana shule, misikiti, vituo vya radio, televisheni na magazeti. Haya  ndiyo mambo mazuri ninayoyasema.

Lakini bado naamini, suluhisho la maendeleo ya Waislamu na Uislamu ni kuwa na taasisi moja (shirikisho) lenye nguvu linalowakilisha kweli matakwa ya Waislamu wote. Hivi sasa hatuna, na matokeo yake ni kama tumegawanywa – na kila mmoja anasema lake, hakuna mwenye mamlaka kwa wengine wala hatuna kauli moja katika masuala muhimu ya kitaifa. 


Fullhabari: Unatathmini vipi ushirikishwaji wa taasisi za Kiislamu katika shughuli za kitaifa?

Sheikh Ponda: Ushirikishwaji wa taasisi nyingine za Kiislamu katika shughuli za kitaifa siyo mzuri sana kutokana na mtizamo wa serikali. Wenyewe wanadhani kuwa, Waislamu wana taasisi moja inayowakilisha mawazo ya Waislamu wote, wakati hilo siyo kweli. Nadhani serikali ikitaka kupata sauti ya Waislamu wote wanapaswa kuwasiliana na taasisi zote zilizopo kwa sababu nazo zimesajiliwa na zina nguvu ya kisheria.

Kuitambua taasisi moja na kuipa nafasi ya kipaumbele siyo sahihi, Sisi Waislamu wa Tanzania bado hatujawa na taasisi moja yenye nguvu inayotuwakilisha wote. Hivyo, hivi sasa, katika masuala ya kitaifa, kila taasisi ambayo imepata usajili inahaki sawa na nyingine bila kujali ukongwe wa mwingine. 

Fullhabari: Tunajua kuwa  wewe ni mdau mkubwa wa kupambania haki za Waislamu katika mambo kadhaa ikiwemo mahakama ya kadhi na mali za Waislamu. Haya  yamefikia wapi? 

Sheikh Ponda: Mahakama ya Kadhi imevurugwa. Sisi tuliandaa andiko juu ya mahakama ya kadhi tunayoitaka, tukamkabidhi Waziri wa Sheria enzi zile, Martin Chikawe. Cha kushangaza licha ya kwamba mchakato ulianzia kwetu, uliporwa, na kupelekwa BAKWATA, na hapo tukapoteza  dira ya kupata mahakama ya kadhi ya kweli, yenye nguvu na inayotambulika kisheria.  
Nadhani walijua kama suala hili lingesimamiwa na viongozi kama vile wa Baraza Kuu au wengineo wasingekubali kuyumbishwa, na wangehakikisha ajenda ya Waislamu inasimamiwa na mahakama ya kadhi ya kweli inapatikana. Hivyo, kuupora mchakato ule halikuwa jambo la bahati mbaya. 

Waislamu hawakuhitaji kuwa na kadhi wa kuziba nafasi, walihitaji kadhi mwenye mamlaka ya kisheria, anayetambulika na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; na bahati mbaya hatuna namna ya kuurejesha mchakato upya kwa sababu tumegawanyika. 

Kuhusu mali za Waislamu (waqf), sipo kimya sana. Suala hilo lilikwenda mahakamani na hukumu tayari ilishatolewa kwamba ni kweli mali za Waislamu ziliuzwa kiholela na iliamuliwa kurudishwa.

Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa John Magufuli kwa kulisema hadharani suala hilo, na kwa nia yake nzuri ya kuzirudisha. Nitumie nafasi hii kumkumbusha Rais wetu mpendwa, anayejali wanyonge atimize ahadi yake kwa Waislamu. Mali zetu bado tunazihitaji kwani ni muda mrefu umepita tangu aahidi. Hali ilivyo sasa siyo nzuri kwa sababu watu bado wanaendelea kutumia mali za Waislamu huku wanatembea kifua mbele.

Fullhabari: Waislamu wanakabiliwa na changamoto gani ambazo 
zinakwamisha maendeleo ya dini yao hapa nchini na duniani kwa ujumla wake?

Sheikh Ponda: Changamoto kubwa hasa ni vitisho nje na ndani ya nchi. Vitisho hivyo vinapelekea watu kuwa waoga, wanashindwa kusimamia haki zao na wapo tayari kusalimu amri hata kama kinachofanyika siyo sahihi. Viongozi wanaoijua dini wapo tayari kuacha kusema ukweli na kusimamia wanachokiamini kwa sababu ya uoga. Ni kwa sababu hii maendeleo ya Waislamu yamekuwa  duni.

Pia viongozi hawako tayari kuutumikia Uislamu, na imefika mahali wanatumia ile falsafa: “Ukishindwa kupambana naye, basi ungana naye.” Viongozi wamekuwa ni watu wa  ndiyo hata kama Uislamu unakandamizwa. Mimi nadhani haiwasaidii. Ni vema wawe na msimamo, na wafuate mafundisho ya Uislamu. Namna hiyo tunaweza kuleta mabadiliko katika dini yetu.  

Lazima viongozi wabadilike na wajione wana jukumu la kuutumikia Uislamu na kumuogopa Allah. Mungu ameshasema hawezi kubadili kitu mpaka watu wenyewe wawe tayari kubadilika. Tusipobadilika, vitisho vitaendelea kutuathiri na maendeleo ya Waislamu na Uislamu hayatapatikana.

Hakuna maoni