Zinazobamba

SHIVYAWATA YAIOMBA SERIKALI IWAWEKEE OFISI HOSPITALI YA MHIMBILI,SOMA HAPO KUJUA

Jengo la Hospitali ya Mhimbili
SHIRIKISHO la Vyama vya Waganga wa Tiba Asili nchini (Shivyawata), limeiomba Serikali kuwapatia jengo katika Hiospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili waweze kutoa huduma za matibabu hasa katika kuunga mifupa.
Rai hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Shivyawata Abdulrahman Lutenga alipozungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kongamano na waganga hao lililokuwa na lengo la kujadili changamoto zinazowakabili katika usajili wa dawa na waganga wenyewe katika Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Alisema kuwa wamekuwa wakishirikiana na serikali katika kutibu wagonjwa kwani kuna wagonjwa wanaoshindikana kutibiwa kwao wamakuwa wakiwapa rufaa ya kwenda katika hospitali za serikali kama MNH na pia wanaoshindikana kutibiwa katika huspitali wamekuwa wakipelekwa kupata huduma kwao.
“Tunaiomba serikali itupatie jingo pale MNH, tuwe tunatoa huduma za matibabu, itakuwa vizuri kama Mgonjwa wa pale kitengo cha mifupa (MOI) akiambiwe apelekwe kwa waganga wa tiba asili,” alisema Lutenga.
 Aidha alibainisha kuwa wagonjwa wamekuwa wakipelekwa kwao kama ‘skrepa’, akiwa na maana kwamba wale walioshindikana kutibiwa na madaktari bingwa ambao alisema kuwa hiyo ni ishara kuwa tiba asili inakubailika nchini.
Alieleza kuwa ni watu  wengi ambao wanaikubali tiba hiyo ambapo alibainisha pia sera ya serikali kutambua uwepo wa tiba asili na kusema kuwa wamekuwa wakishirikiana na serikali.
Alifafanua kuwa Serikali ilitunga sheria, ambayo  inaitambua tiba asili na kwa sasa wanapigania kuundwa kwa kanuni ya kuwatambua waganga waliosajiliwa ili waende kusaidia kuunga mifupa MOI.
Alisema mwezi uliopita shirikisho hilo lilianza kuhakiki wanachama wake ambapo waganga 3500 wamekwisha hakikiwa na kuziomba mnamlaka husika za usajili ziweze kuwasajili.
Aliomba kusiwepo mamlaka yoyote ya serikali itakayoleta vikwazo katika usajili kwani itakuwa na nia mbaya kwa waganga hao kwa kuwazuia kufanya kazi yao ambayo wamekuwa wakifanya kwa muda mrefu.
Alitoa rai Baraza la Usajili wa Tiba Asili inchini kuweka vigezo rahisi ili usajili pia uwe rahisi, alibainisha kuwa endepo mganga mwenye vigezo hatasajiliwa wao kama shirikisho hawatamzuia kufanya kazi yake.
Aidha kutokana na kuwepo kwa sinto fahamu baina yao na Baraza la Usajili wa Tiba Asili na Tiba Mbadala aliwataka waganga wote nchini kuwa watulivu katika wakati huu ambao wanajaribu kutafuta ufumbuzi wa jinsi ya kuwezesha usajili wa waganga na dawa zao pasipo vikwazo.