Zinazobamba

SERIKALI YAVIBANA VYUO VIKUU,NI VILE VINAVYOTOZA ADA KWA FEDHA ZA KIGENI,SOMA HAPO KUJUA



 
Vyuo Vikuu hapa Nchini vimeagizwa kuacha mara moja kutoza ada kwa fedha za kigeni kwa wanafunzi ambao ni watanzania.

Agizo hilo limetolewa leo Bungeni, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Elimu,  Sayansi na Teknolojia Mhandisi Stella Manyanya alipokuwa akijibu swali  lililoulizwa na Mbunge Jaku Hashimu Ayoub kwamba kumekuwa na malalamiko  ya wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania ambao ni wazawa kulipishwa ada ya  masomo yao kwa fedha za kigeni badala ya fedha za Kitanzania.

“Sarafu inayotakiwa kutumika Tanzania ni shilingi ya Kitanzania kwa mujibu wa  kifungu cha 25 na 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ya mwaka 2006. Aidha, kwa Tanzania malipo ya kitu au huduma yoyote inapaswa  kulipwa kwa shilingi ya Kitanzania kama ilivyoainishwa kwenye kifungu cha 28 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, 2006,” alifafanua Mhandisi
Manyanya.

Aliendelea kwa kusema kuwa japo Wizara haijapokea
malalamiko yoyote ya kutozwa fedha za kigeni kwa wanafunzi wa Elimu ya  Juu tangu itoe agizo kama hilo kwa wamiliki wa vyuo Septemba 07, 2016.

Hivyo basi kwa mara nyingine Mhandisi Manyanya ameviagiza vyuo ambavyo bado  vinatoza wanafunzi Watanzania fedha za kigeni kuacha mara moja kwani  vyuo hivyo vimeelekezwa kutoza wananchi wa Kitanzania kwa pesa ya  Kitanzania.

Aidha Mhandisi Manyanya amewataka watanzania kutoa
taarifa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwa kuna Chuo chochote  kinachotoza ada kwa Watanzania kwa fedha za Kigeni ili hatua stahiki za  kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.