Zinazobamba

TAKUKURU KINONDONI YAFUATILIA MIRADI YA SHILINGI BILIONI MBILI OKTOBA HADI DESEMBA 2024

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Christian Nyakizee.

-Yawaomba Wananchi kuendelea kutoa ushirikiano.

-Yajipanga kupambana na rushwa Uchaguzi Mkuu 2025.

Na Mussa Augustine.

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kufuatilia miradi mitano yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.8 katika kipindi cha Mwezi Oktoba hadi Desemba 2024.

Taarifa hiyo imetolewa leo Februari 6 2025 Jijini Dar es salaam na Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni Bw.Christian Nyakizee wakati akizungumza na Waandishi wa habari Ofisini kwake.

Aidha Nyakizee amefafanua kuwa miradi hiyo imehusu Sekta ya Elimu na Ujenzi nakwamba kati ya miradi hiyo miradi miwili yenye thamani ya shilingi milioni 144.8 imekutwa na mapungufu madogo madogo ambapo wahusika wameshauriwa kurekebisha mapungufu hayo na ufuatiliaji utafanyika kuhakikisha wamefanyia kazi ushauri uliotolewa

Pia amesema kuwa mradi mmoja wa ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa katika shule ya msingi Ubungo NHC wenye thamani ya shilingi milioni tisini (90,000,000/=)ulibainika kubadilishwa kazi iliyotolewa awali ,ambapo amesema kibali kilichotolewa kilikua nicha kufanya ukarabati wa majengo ya madarasa nabadala yake wakaanzisha ujenzi waadarasa mapya.

Aidha amesema kwamba taasisi hiyo imefanya mambo mbalimbali ikiwemo uchambuzi wa mifumo ili kubaini mianya ya rushwa katika maeneo ya kiutendaji ya Ofisi,taasisi au miradi mbalimbali na kudhibiti,pamoja na kufanya uchambuzi wa mifumo ya uodoshaji taka ngumu ngazi ya kaya na maeneo ya Biashara katika Manispaa ya Kinondoni.

"Pia tulifanya uchambuzi wa mfumo wa usimamizi na ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki (POS) katika Manispaa ya Ubungo,Uwasilishaji michango mifuko ya hifadhi ya Jamii katika halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni pamoja na usomaji Mita na Ankara za Maji DAWASA Wilaya ya Ubungo".

Nakuongeza kuwa,"kwa upande wa uelimishaji umma tumefanya semina  sitini na moja(61),Mijadala ya wazi miwili(2),Mikutano ya hadhara thelathini  na mbili(32)Uandishi wa Makala tatu(3),Vipindi vya radio na Tv 06,kuimarisha klabu za wapinga rushwa ishirini na sita(26)na Mdahalo mmoja (1)." 

Aidha Mkuu huyo wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni amesema taasisi hiyo imepokea jumla ya malalamiko 85 na kati ya hayo malalamiko 46 yamehusiana na vitendo vya rushwa huku malalamiko 39 yakihusu masuala  mengine ikiwemo migogoro ya ardhi.

"Malalamiko ambayo hayakuhusu rushwa walalamikaji wengine wameshauriwa na majalada kufungwa na wengine wameelekezwa sehemu sahihi ya kupeleka malalamiko yao,kwa malalamiko yanayohusu rushwa majalada yanaendelea kushughulikiwa na yapo katika hatua mbalimbali" amesema Nyakizee

Halikadhalika amebainisha  kuwa  katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2024 wamefanikiwa kufungua Mashauri mapya yapatayo sita katika Mahakama ya Kinondoni na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo,nakwamba Jamhuri imeshinda Mashauri mawili ,huku Mashauri 27 yanaendelea mahakamani.

Pia amesema kupitia maadhimisho ya siku ya maadili na haki za binadamu taasisi hiyo imeendesha warsha kwa Watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwananyamala kuhusu umuhimu wa Maadili ,Madhara ya rushwa ya ngono katika jamii nakuwataka Watumishi kuchukua hatua kukabiliana na tatizo kwa kutokuchukua rushwa ili kuficha ukweli wanapotakiwa kuthibitisha kiafya endapo tuhuma inayolalamikiwa imefanyika ama vinginevyo ili watuhumiwa kuweza kuchukuliwa hatua.

Katika hatua nyingine Nyakizee amesema kwamba Wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 taasisi hiyo ilielimisha wananchi kuhusu Madhara ya rushwa kipindi cha uchaguzi pamoja na kuwahamasisha kushirikiana na TAKUKURU kutokomeza rushwa katika kipindi chote kabla ya uchaguzi ,wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.

Hata hivyo emesema kuwa Taasisi yake imejipanga kuendelea kuhamasisha Wananchi kushirikiana na TAKUKURU katika kuelekea kwenye maandalizi ya uchaguzi Mkuu wa 2025 wa Madiwani,Wabunge na Rais.

"Tunaendelea kutoa wito kwa Wananchi wote katika Mkoa Wetu waendelee kutoa ushirikiano kwa TAKUKURU na kuwasihi kuwa wapatao taarifa zozote za rushwa wawasiliane nasi bure kwa kupiga au kutuma ujumbe mfupi kwa namba ya dhalura 113 na kufuata maelekezo au kufika katika Ofisi yoyote ya TAKUKURU iliyopo karibu nao" amesisitiza Nyakizee


Hakuna maoni