Serikali yatangaza ‘Diploma’ ndiyo kigezo cha chini cha elimu kwa waandishi wa habari
Serikali imetangaza kuwa kiwango cha chini cha
taaluma anayopaswa kuwa nayo mwandishi wa habri kuwa ni 'Diploma ya Uandishi wa
Habari' kwa mujibu wa kanuni za sheria mpya ya hunda za habari zilizokamilika
utungaji wake hivi karibuni.
Akizungumza na wana habari leo mjini Dodoma, Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo , Nape Nnauye amesema kuwa kanuni
zimeshaundwa na zimechapishwa kwenye gazeti la serikali tangu Februari 3 mwaka
huu baada ya kupokea maoni ya wadau mbalimbali.
"Tumesoma, tumechambua maoni ya
wengi, wapo waliotaka iwe cheti, wengine diploma, wengine digrii, wapo
waliotaka PhD na wapo waliotaka iwe mtu yeyote nayejua tu kusoma na kuandika.
Serikali imesimama katikati ya maoni hayo. Sifa ya chini kabisa kwa kuanzia
itakuwa ni diploma ya uandishi wa habari” Amesema Nape
Waziri Nape amesema pia kuwa sheria hiyo imeshaanza
kutumika tangu Desemba 31 mwaka 2016, ambapo yeye kama Waziri mwenye dhamana
alishatoa tangazo katika gazeti la serikali.
Aidha kuhusu wasio na sifa hiyo, Waziri Nape amesema
kuwa serikali imetoa kipindi cha mpito cha miaka mitano ili waandishi wasiokuwa
na sifa hiyo, waliopo sasa na watakaoingia kwenye taaluma hiyo, wakasome ili
wawe wamepata sifa hiyo.
Amesema katika utekelezaji wa sheria hiyo, kuna
taasisi ambazo tayari zipo, zitaongezewa majukumu au kazi zake kuhuishwa, pia
kuna vyombo vipya vitaanzishwa na kuna taratibu mpya za kiutendaji
zitaandaliwa.
Kuhusu manufaa ya sheria hiyo, Nape amesema kuanza
kutumika kwa sheria hiyo ni jambo muhimu kwa tasnia hiyo kwa kuwa ni ruhusa ya
kuanza kwa mchakato wa kuifanya taaluma ya habari kuwa taaluma kamili yenye
sifa mahsusi na maadili yaliyokamilika pamoja na kuwa na vyombo vya
kusaidia utekelezaji wake.
Sheria hiyo ilisainiwa na Rais Magufuli Novemba 16
mwaka 2016, na siku mbili baadaye ilichapishwa kwenye gazeti la serikali baada
ya muswada wake kupitishwa na Mkutano wa 5 wa bunge mwezi Novemba 2016.