WAZIRI TIZEBA AFUNGUKA KUHUSU SAKATA LA BALAA LA NJAA,SOMA HAPO KUJUA
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles
Tizeba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji wa chakula
nchini leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mhandisi
Mathew Mtigumwe.
|
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Dkt. Charles
Tizeba amelazimika kutoa ufafanuzi kuhusu hali ya chakula nchini huku
akisisitiza kuwa Tanzania ina chakula cha kutosha na haina njaa kabisa.
Dkt. Tizeba ametoa ufafanuzi huo leo wakati akiongea
na waandishi wa habari, na kusema kuwa watu wanaoneza taarifa za kuwepo kwa
njaa Tanzania wana lengo la kuingiza mahindi yao yasiyo na ubora ili wafanye
biashara, jambo ambalo serikali imelikataa.
Akizungumzia uhalisia wa hali, amesema kilichotokea
ni kupanda kwa bei ya mahindi, hali iliyosababishwa na uamuzi wa serikali kuuza
nafaka hiyo katika mataifa jirani yaliyokuwa na uhitaji mkubwa, ingawa kiwango
kilichouzwa kilikuwa ni sehemu ya mahindi ya ziada.
"Mwaka jana gunia la mahindi kwa
bei ya wastani wa kitaifa ilikuwa 65,000 lakini sasa ni 85,000 na wala
haijafikia mara mbili mara tatu kama inavyosemwa ingawa kuna maeneo kama rorya
imefikia hadi 150,000 kutokana na wao kutegemea misimu miwili wakajikuta
wanatumia akiba yao lakini hali ya hewa ikawa tofauti kwahiyo kuna
wafanyabishara wakaamua kutumia hiyo fursa kupandisha bei zaidi" Amesema.
Ameendelea kusema ..... "Mavuno ya nafaka
yalikuwa tani milioni 16 wakati mahitaji yakiwa tani milioni 13 kwahiyo ziada
ilikuwa tani milioni 3, kwahiyo katika hiyo ziada milioni 1.5 ikasafirishwa
nje, wenzetu walikuwa wananunua kwa gharama yoyote kwa kuwa walikuwa na shida,
hiyo ndiyo maana bei ya nafaka imepanda sana hasa mahindi, kwa sasa bei imefika
hadi mia 8 mia 9 na wauzaji ni walewale, kwahiyo hawezi kuuza ndani kwa bei ya
chini lakini kupanda huko kulitarajiwa"
Amesema kupanda bei kwa mahindi kulitarajiwa na ni
kwa kawaida na wala hakuwezi kumaanisha kuwa Tanzania kuna njaa wakati nafaka
zote zinapatikana kila kona ya Tanzania
"Hakuna soko halina mahindi, hakuna
soko halina mchele, hakuna soko halina maharage, masoko ya mijini yamejaa
viazi..... nchi ina ziada tani milioni 3 kwanini mnataka tukanunue tena tani
milioni 1 za nini?"
Kuhusu ukame, amesema ni kweli kuna hali ya upungufu
wa mvua, na hiyo inafahamika maana ilishatabiriwa na kuwataka wananchi watunze
akiba yao ya chakula na wasidanganyike kukiuza, kwa sababu hali ya hewa
haitakuwa nzuri katika baadhi ya maeneo.
Amewasihi wananchi waache tamaduni ya kung'ang'ania
chakula cha aina moja na kuwataka kutumia mchele na viazi kama wanaona mahindi yamepanda
bei.. "Nafaka siyo mahindi tu, tunao mchele na mpunga wa kutosha, na
viazi vipo kutoka Tunduma, watumie hivyo"
Waziri huyo amepiga marufuku mtu yoyote kutoa
taarifa za njaa kwa kuwa serikali ndiyo inayojua hali ya chakula kupitia vyanzo
vyake.