WAFUGAJI 50 WALA KINYESI,DAMU NA MKOJO KUNUSURU MAISHA YAO,SOMA HAPO KUJUA
Watu
50 wakiwa na watoto wadogo wamenusurika kufa, baada ya kupotea ndani ya
Pori la Akiba la Selous kwa siku saba; huku wakikosa chakula na maji na
kulazimika kula kinyesi cha ng’ombe, damu na mikojo ya binadamu.
Watu
hao ambao ni wafugaji, walikuwa wakihama na mifugo yao inayokadiriwa
kufikia 1,780 kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Rufiji mkoani Pwani,
yakiwemo Chumvi na Muhoro waliekea Morogoro, ambako walidai ndiko
yalipo makazi yao.
Tukio
hilo ambalo si la kawaida kutokea katika pori hilo, lilianzia Jumatano
iliyopita wakati wafugaji hao, walipoanza safari ya kuelekea Malinyi
mkoani Morogoro, wakiongozwa na mwenyeji wao, waliyemtaja kwa jina la
Mzee Mzigua, ambaye hata hivyo wanadai aliwalaghai na kuwatelekeza.
Wafugaji
hao walisema walitembea kwa siku tano ndani ya pori hilo, wakitarajia
kufika Malinyi, yaliko makazi yao. Lakini hali ilikuwa tofauti, baada ya
mwenyeji wao huyo, kuwalaghai kwa kuwapitisha njia sisizo sahihi.
Walisema
waliishiwa chakula na maji ya akiba na mwisho walijikuta wanatokea
ndani ya Pori la Akiba la Selous; huku hali zao zikiwa zimedhoofu
kutokana na njaa na kiu cha maji. Wakiwa safarini, mwenyeji wao huyo,
aliwataka kila mmoja alipe fedha ikiwa ni ujira wake kwa kuwaonyesha
njia. Walidai kuwa walimlipa fedha nyingi.
Wengine
walimlipa Sh milioni mbili, Sh milioni moja na wengine Sh 500,000,
wakitarajia angewasaidia. Walitembea usiku na mchana ndani ya pori hilo,
wakipishana na wanyama wakali kama simba na nyati, hivyo kuhatarisha
usalama wa maisha yao na watoto wao.
Hali
ilizidi kuwa mbaya zaidi, baada ya kutimia siku ya tano wakiwa ndani ya
pori hilo, pale walipoishiwa chakula na maji, hivyo kuwalazimu kuanza
kuchinja ng’ombe na kunywa damu kwaajili ya kukata kiu. Pia walikula
kinyesi chao ili kupunguza njaa. Yule mwenyeji wao aliwatelekeza baada
ya kuona hali zao zimekuwa mbaya.
Alitokomea
kusikojulikana, akiwaacha wasijue pa kwenda, hivyo kulazimika
kutelekeza mifugo yao ili kunusuru kwanza maisha yao. Halikadhalika,
wengine walilazimika kunywa mikojo yao na mingine kuwanywesha watoto wao
kunusuru maisha yao, hali iliyowafanya kuathirika kiafya na kushindwa
kuendelea na safari.
Wengine walianguka na kupoteza fahamu. “Sisi
tulikuwa tunataka turudi nyumbani kwetu Morogoro. Huku tulikuja wakati
wa operesheni ya Morogoro, huku tulikuja kununua ng’ombe lakini miji
yetu ipo kule Morogoro. Tukaambatana na huyo mwenyeji wetu
aliyejitambulisha kwa jina la Mzee Mzigua na mtoto wake.Lakini tunajua
mpaka nyumbani kwake”alisema Kiongozi wa msafara wa wafugaji hao, aliyejitambulisha kwa jina la Lisesi Cherahani Bela na kuendelea;
“Zilitimia
kama siku nne tukiwa hatujanywa maji, jua lilikuwa linawaka, tukaanza
kuanguka, tukaanza kuchinja ng’ombe na kunywa damu, tulijaribisha kula
kinyesi cha ng’ombe, tulikuwa tunakojoa mkojo tunanywesha hata watoto.
Mimi nilikunywa mkojo lita moja, ikaniathiri hapa kifuani, kumbe mkojo
ni kitu kibaya.”
Akizungumza
na waandishi wa habari waliofika katika eneo hilo, kiongozi huyo
alisema baada ya kuona hali inakuwa mbaya zaidi, alitafuta eneo ambalo
lina mtandao wa simu na kufanya mawasiliano na watu mbalimbali, ambapo
alifanikiwa kuwasiliana na watu wa Kigoma na kuomba msaada wao.
Alisema
kuwa watu hao, waliwasiliana na wahifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi
na kuwasiliana na wahifadhi wa Pori hilo la Selous, ambao walianza kazi
ya kuwasaka na hatimaye kuwakuta katika eneo la Mlima Luhombelo,
lililopo katikati ya Pori hilo wakiwa tayari wameshadhoofika kiafya.
Askari
hao wa wanyamapori wa Pori hilo, waliwapatia uji na maji na kuwapa
huduma ya kwanza wale wengine ambao walikuwa na hali mbaya.
Baada
ya taarifa hizo za kupotea kwa wafugaji hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Maliasili na Utalii, Gaudence Milanzi alifika katika eneo hilo juzi,
akiambatana na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Wanyamapori Tanzania
(TAWA), Martin Leibooki, Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Henock
Msocha na maofisa wengine wa wizara na pori hilo.
Milanzi
alisema Serikali inaangalia namna ya kuwasaidia wafugaji hao, kurejea
katika hali zao kiafya pamoja na kuwasaidia kutafuta mifugo yao ili
waweze kurejea katika makazi yao na kuendelea na shughuli zao.
“Kwa
upande wa Serikali kama Wizara hatuchukulii kama hawa wameingia kwenye
hifadhi hapana, muhimu kwanza ni kuokoa maisha ya binadamu, na hicho
ndicho tunategemea kukifanya sasa hivi, na baada ya hapo kutakuwa na
masuala ya kutafuta hiyo mifugo, kwa sababu wamepata hasara kubwa”alisema Katibu Mkuu huyo.
Aliutaka
uongozi wa wilaya ya Rufiji, kutoa ushirikiano na wizara ili kuwabaini
waliowadanganya wafugaji hao, kwa kuwaingiza kwenye pori hilo na
kuwatapeli kiasi hicho kikubwa cha fedha.
“Hawa
waliowadanganya na kupita huko ndani ya pori kwa kweli tutaendelea
kuwatafuta na tutaomba tuwe na ushirikiano na uongozi wa Wilaya kwa
sababu inaelekea kuna watu kazi yao ndo hiyo, ukiangalia pesa walizowapa
ni nyingi sana, sasa watu wamechukua pesa zote na wamewaacha katika
hali kama hii, wengine wana watoto wadogo, kwa hiyo tutahakikisha
tunashirikiana kuwatafuta ili tukomeshe hili tatizo moja kwa moja”alisema.
Katibu
Mkuu huyo alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa TAWA na Mhifadhi Selous kwa
juhudi za haraka walizochukua. Alisema wizara yake itaendelea
kushirikiana na Mamlaka mbalimbali, kutoa misaada ya haraka, endapo
yatatokea tena matukio ya aina hiyo.
Kwa
upande wake, Leibooki alisema TAWA ambao ndiyo wamiliki wa hifadhi zote
za wanyamapori nchini, haitawachukulia hatua za kisheria wafugaji hao,
kwa kuwa waliingia ndani ya pori kwa kudanganywa na watu wenye nia
mbaya.
Lakini,
alisisitiza kuwa mamlaka yake, itawashughulikia kisheria wawindaji
haramu na wafugaji wanaoingiza mifugo yao ndani ya hifadhi zilizo chini
ya Mamlaka yake.
Pia
alisema Mamlaka yake, inaendelea na utaratibu wa kushirikiana na
wananchi waishio pembezeni mwa hifadhi zote, kwa kuwapa elimu ya ufugaji
bora kwa kushirikiana na wizara zinazohusika na kuendeleza miradi ya
maendeleo, ikiwemo miundombinu ya maji.
Katibu
Mkuu wa Chama cha Wafugaji chini (CCWT), Magembe Makoye aliwataka
viongozi wa Halmashauri mbalimbali nchini, kutatua migogoro ya wakulima
na wafugaji mahali walipo, bila ya kuondoa watu wengine.
Alisema
kuwa wao kama chama, wamesikitishwa na tukio la kuondolewa kwa wafugaji
hao katika bonde hilo la Rufiji, kwa kuwaambia warudi walipotoka.
Alisema tamko hilo lilitolewa na uongozi wa Halmashauri hiyo na ndilo
lililosababisha matatizo hayo.
Makoye
alisema kufanya hivyo, hakuondoi migogoro ya wafugaji na wakulima,
badala yake ni kuendelea kuzalisha migogoro hiyo katika maeneo mengine,
ambayo wafugaji watahamia.
“Tunalaani
kweli vitendo hivi vya viongozi na watendaji wengine wa Halmashauri
kuwafukuza wafugaji, tena wakati mwingine kwa kuwatisha na matokeo yake
wananchi hawa 50 wangepoteza maisha, kama isingekuwa bahati ya mtu mmoja
kuwa na simu kati yao” alisema Katibu Mkuu huyo.
“Kwa
kweli kwa niaba ya wafugaji wote wa Tanzania naishukuru sana Wizara ya
Maliasili kupitia kwa Katibu Mkuu, Gaudence Milanzi.” alisema Katibu huyo.
Alisema
kuwa kungeweza kutokea majanga makubwa zaidi kwa kuwa kuwa wafugaji hao
walikuwa wakisafiri na watoto wao wadogo katika mazingira hatarishi
katikati ya pori hilo, ambalo lina wanyama wakali.
“Kwa
kweli ni mazingira ya kusikitisha. Lakini niishukuru sana Serikali kwa
maana ya Wizara ya Maliasili na Utalii, wamefanya kazi yao kwa namna
ambavyo mimi ninawiwa kuwashukuru. Tangu jana tumewasiliana na Katibu
Mkuu wa Wizara, leo watu wote wameweza kupatikana, kumefanyika doria ya
ndege, doria za magari, doria kwa miguu, wamewatafuta hawa watu,
wamewaokoa, wamewaleta kwenye huduma za afya, wamewapa chakula,
wamewahifadhi, hawajawadhuru” alisema.
Baadhi
ya Mzoga wa ngombe uliopatikana ndani ya Pori la Akiba la Selous,
Kanda ya Kaskazini Mashariki Kingupira baada ya Wafugaji 50
waliotelekezwa kwa muda wa siku tano na mtu mmoja waliyemtaja kwa jina
maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia za mkato ndani ya
Pori hilo na kisha kuwakimbia( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya
Maliasili na Utalii)
Mmoja
wa wafugaji aliyepotea na kutelekezwa ndani ya Pori la Akiba la
Selous, Bw. Lisesi Cherehani aliyekuwa na ng’ombe 180 na punda mmoja
akiangalia mmoja wa ng'ombe wake aliyekufa kwa kukosa maji ya kunywa
kwa muda wa siku tano kwenye Kanda ya Kaskazini Mashariki katika Pori
la Akiba la Selous ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya Maliasili na
Utalii)
Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi
(katikati) akipata taarifa kutoka kwa Meneja wa Mradi wa Pori la Akiba
la Selous Bw. Enock Msocha (wa tatu kushoto) mara baada ya kuwasili
kwa ajili ya kuwatembelea Wafugaji 50 waliokolewa na Askari
wanyamapori baada ya kutelekezwa na mtu mmoja waliyemtaja kwa jina
maarufu la Mzigua aliyewarubuni kwa kuwaonyesha njia ya mkato ndani ya
Pori hilo na kisha kuwakimbia ( Picha na Lusungu Helela-Wizara ya
Maliasili na Utalii)