BALAA LA NJAA LINALOLINYEMELEA TAIFA,MBUNGE ZITTO KABWE AIBANA SERIKALI VIBAYA,SOMA HAPO KUJUA
Kiongozi wa Chama cha ACT –Wazalendo, Zitto Kabwe
ameitaka Serikali kutangaza rasmi baa la njaa kwa mujibu wa sheria kutokana na
hali ya chakula kuwa mbaya nchini.
Kauli ya Zitto imetolewa wakati Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa akisisitiza utunzaji wa chakula baada ya kukagua maghala ya nafaka
yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya
Songea.
Agizo la Majaliwa pia limetolewa siku mbili baada ya
Waziri wa Kilimo, Dk Charles Tizeba kutofautiana na Zitto kuhusu hali ya
chakula ambapo Waziri huyo alisema hali ya chakula nchini ni shwari huku Mbunge
huyo wa Kigoma Mjini akisema ni mbaya.
Jana, mbunge huyo akihutubia mkutano wa kampeni ya
kumnadi mgombea udiwani Kata ya Nkome, Geita aliendelea kupigilia msumari kauli
yake akisema, “Hali ya chakula ni mbaya, ni mbaya, ni mbaya.”
Alisema baada ya ziara ya Waziri Mkuu kwenye maghala
ya Taifa na kujionea hali ya chakula nchini, ni vyema Serikali ikachukua hatua.
“Ninapendekeza Serikali ichukue hatua
muhimu ya kisheria ya kutangaza baa la njaa nchini. Tamko la baa la njaa
litaisaidia Serikali kupata bajeti ya dharura ya kununua chakula na kutoa uhuru
kwa wakuu wa wilaya kutangaza bila woga kuwa maeneo yao yana njaa,” alisema
Zitto huku akimpongeza Majaliwa kwa ziara hiyo.