MAFURIKO YA LOWASSA SASA KUAANZA KUREJEA TENA,SOMAHAPO KUJUA
Wanasiasa wakongwe nchini, Maalim Seif Sharif Hamad
aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na Edward Lowassa aliyekuwa
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , kesho wanatarajiwa kuungana
kwa mara ya kwanza jukwaani tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Vigogo hao wa vyama vya CUF (Maalim Seif) na Chadema
(Lowassa) wataunguruma katika viwanja vya Skuli ya Fuoni visiwani Zanzibar
kumnadi mgombea ubunge wa jimbo la Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib
Ramadhani, katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januri 22 kuziba nafasi ya
aliyekua mbunge wa jimbo hilo, Hafidh Ally Tahir aliyefariki dunia Novemba
11 mwaka jana.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu
amesema kuwa chama chake kimemua kuungana na CUF katika uchaguzi huo ili
kuhakikisha mshirika wake huyo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
anamshinda mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, Mwalimu aliongeza kuwa baada ya Lowassa
kushiriki uzinduzi wa kampeni hizo kesho, viongozi wengine wa Chadema watafuata
kwa kufanya mikutano mbalimbali jimboni humo. Alisema kuwa baada ya Lowassa
atafuata Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe pamoja Tundu Lissu kwa
nyakati tofauti, kisha wengine wataendelea hadi mwisho wa kampeni hizo.
Akizungumzia uamuzi huo wa Chadema, Mkurugenzi wa
Habari,Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, Salim Bimani alieleza kufurahishwa na
uamuzi huo wa Chadema na kueleza kuwa hatua ya Lowassa kuhudhuria uzinduzi huo
itaongeza hamasa kubwa kwa wapenzi wa chama hicho.
“Umenambia hadi Lowassa atakuwepo? Ni furaha
iliyoje, Wanzibari wana shauku kumuona. Siku ya kampeni patakuwa hapatoshi
Skuli ya Fuoni, hapa Simba (Maalim Seif) kule Lowassa kipenzi kingine cha
Wazanzibar,” Bimani anakaririwa na Mwananchi.
Aliongeza kuwa kama Lowassa atahudhuria mkutano huo
atakuwa na mambo mawili makubwa ya kufanya, la kwanza likiwa kuwashukuru
Wazanzibar kwa kura walizompa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka jana. Na la pili
litakuwa kumpigia kampeni mgombea wa CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhani.
Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema na
Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF, wataingia katika jimbo hilo ikiwa ni
siku chache baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kufanya uzinduzi wa
kampeni hizo akiambatana na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho.
Hivyo, kwa muktadha wa kisiasa, vigogo hao wa Ukawa
wana kazi ya kusawazisha matuta yaliyowekwa na timu ya chama tawala
iliyoongozwa na Kinana.