TANESCO BADO KWAFUKUTA TU,HOMA YAZIDI WANYEMELEA VIGOGO,SOMA HAPO KUJUA
Siku moja baada ya vigogo watatu wa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco) kushushwa vyeo, uongozi wa shirika hilo umesema utaendelea
na fagio hilo kama njia ya kuongeza ufanisi kwenye utendaji.
Vigogo hao wa ngazi za juu ambao ni wakurugenzi,
wamehamishiwa Chuo cha Mafunzo cha Tanesco (TSS) kwa madai kuwa shirika
linaboresha ufanisi wake.
Walioshushwa vyeo ni pamoja na Declan Mhaiki
aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia usambazaji wa umeme.
Wengine ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji na
Huduma kwa Mteja, Mhandisi Sophia Mgonja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji
Uzalishaji Umeme, Nazir Kachwamba.
Wakati hao wakipitiwa na panga hilo, Mkurugenzi wa
Idara ya Rasilimali Watu, Watson Mwakyusa, aliamua kuandika barua kuacha kazi
mwenyewe.
Juzi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito
Mwinuka, alisema jana wangetoa taarifa kuhusu hamisha hamisha hiyo.
Jana mchana Idara ya Kitengo cha Mahusiano cha
Shirika hilo, kilitoa taarifa na kusema kuwa wataendelea na hatua mbalimbali za
mabadiliko ya uongozi kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi wa kiutendaji.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mabadiliko yanayoendelea
ndani ya Tanesco yatawekwa wazi wakati mwafaka kwa mujibu wa sheria, kanuni na
taratibu za shirika kupitia vyombo vya habari.
Kitengo hicho kilieleza kuwa kwa sasa bado wanaendelea
na panga pangua na endapo watakamilisha watatoa taarifa kwa umma.
“Tunaomba vyombo vya habari vitoe fursa
kwa mamlaka husika kuendelea kukamilisha zoezi hili muhimu kwa maendeleo ya
Shirika na Taifa kwa ujumla na taarifa rasmi itatolewa baada ya zoezi
kukamilika,’’ ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Januari Mosi, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli
alimteua Dk. Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, baada ya
kumng’oa aliyekuwa mkurugenzi wa shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba.
Mramba alitenguliwa uteuzi wake siku mbili baada ya
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kutangaza kuridhia
ombi la Tanesco la kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 kutoka 18
waliyoomba.
Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mwinuka alikuwa Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akiwa mjini Bukoba kwenye ibada ya Mwaka Mpya, Rais
Magufuli alisema amekerwa na kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa
umma kujitokeza hadharani na kutangaza au kuzungumzia mambo ya kitaifa kama
uamuzi wa Serikali bila kushirikisha viongozi wao wa ngazi za juu.
Kutokana na hali hiyo, alisema watendaji hao ni
miongoni mwa majipu yanayostahili kutumbuliwa.