JINA LA LOWASSA LATAJWA KWENYE DENI LA MILIONI 1,SOMA HAPO KUJUA
Jina la waziri mkuu mstaafu, Edward Lowassa
limetajwa na mkaazi mmoja wa Mbeya mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla kuwa
sababu ya deni la shilingi milioni moja kutokana na mapenzi ya wafuasi wake.
Mkaazi huyo wa kata ya Ruanda Nzovwe
aliyejitambulisha kwa jina la Amos Mwakyambiki alidai kuwa wafuasi wa Chadema
waliharibu paa la nyumba yake walipopanda kwa lengo la kufuatilia mkutano wa
Lowassa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, na kwamba chama hicho kilimuahidi
kumlipa fidia ya shilingi milioni moja lakini hadi sasa ahadi hiyo
haijatekelezwa.
Alimueleza mkuu wa mkoa huo kuwa kutokana na
uharibifu huo mkubwa uliofanyika, wapangaji wake waliamua kuhama nyumba yake
hivyo kukosa kipato.
“Naomba Serikali ya Mkoa inisaidie kuzungumza na
meya (wa Chadema) ili niweze kulipwa stahiki zangu kwani sasa sijui hatma
yangu. Kuku niliokuwa nauza kwa ajili ya kupata nauli kwenda ofisi za jiji
wamekwisha,” Mkaazi huyo anakaririwa.
Kutokana na madai hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya
alimuagiza Mkuu wa Wilaya kufuatilia suala hilo huku akitahadharisha wananchi
kuhusu matumizi ya nyumba zao wakati wa kampeni.
“Lakini na nyie wananchi msikubali nyumba zenu
zibadilishwe kuwa viwanja vya siasa,” alisema Makalla.
Akizungumzia taarifa hizo, Mkuu wa Idara ya Habari
ya Chadema, Tumaini Makele alisema kuwa chama hicho kitafuatilia kuona ni nani
aliyetoa ahadi hiyo kwa mwananchi huyo na ilikuwa katika mazingira gani ili
walifanyie kazi ipasavyo.