TAARIFA: Kukanusha Taarifa Iliyoandikwa Na Gazeti La Raia Mwema Kuhusu Kuongezwa Muda Wa Leseni Za Vitalu Vya Uwindaji Bila Kufuata Taratibu

Wizara ya Maliasili na Utalii inakanusha taarifa
iliyoandikwa na gazeti la Raia Mwema Toleo Na. 494 (ISSN 1821-6250) la Jumatano
tarehe 25-31 Januari, 2017 ikiwa na kichwa cha habari “Waziri Maghembe
Matatani”. Habari hiyo imeeleza kuwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof.
Jumanne Maghembe anadaiwa kuongeza muda wa leseni za vitalu vya uwindaji kwa
kampuni za uwindaji wa kitalii kinyume na taratibu.
Aidha, habari hiyo imeeleza kuwa waziri hakufuata
utaratibu uliowekwa katika kifungu cha 38 (6) cha Sheria ya Uhifadhi
Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 ambayo inaweka utaratibu wa kufuatwa kabla
waziri hajatoa leseni upya. Pa, habari hiyo imeeleza kuwa sheria hiyo inataka
itangazwe kwenye magazeti utaratibu wa kuomba vitalu kwa waombaji pamoja na
kufanyiwa tathmini.
Vilevile, habari hiyo imeeleza kuwa waziri anatakiwa
kushauriwa na chombo ambacho ndicho hufanyia tathmini kampuni hizo. Taarifa
hiyo imeripoti kuwa hapo awali kulikuwa na kamati ya kumshauri waziri ambayo
ilivunjwa mwaka 2012 na aliyekuwa waziri wa Wizara hiyo, Khamis Kagasheki na
hivyo kuhoji uhalali wa kufanya maamuzi bila kushauriwa na chombo hicho.
Habari hiyo siyo ya kweli, kwani Waziri hakutoa
leseni za umiliki wa vitalu vipya bali ameongeza muda wa umiliki wa vitalu kwa
mujibu wa kifungu cha 38 (8) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka
2009 sambamba na kanuni ya 16 ya Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za mwaka 2015.
Sheria na Kanuni hiyo inaelezea utaratibu wa kuongeza muda wa umiliki wa vitalu
kwa wale walioomba kuendelea na umiliki wa vitalu vya awali (renewal of hunting
block).
Waziri kabla ya kuongeza muda wa umiliki wa vitalu
(renewal) alikaribisha maombi kwa wale wanaotaka kuongezewa muda wa umiliki wa
vitalu wanavyovimiliki kwa mujibu wa Sheria tajwa hapo juu kwa barua yenye
Kumb. Na. CHA.79/519/47 ya terehe 22 Aprili, 2016. Aidha maombi hayo yalipitiwa
na Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji ambayo ipo kisheria na
iliteuliwa Septemba 2013, kinyume na madai ya mwandishi kuwa Kamati hiyo haipo.
Baada ya tathmini ya maombi hayo, Kamati hiyo ilimshauri Waziri kwa mujibu wa
sheria.
Kwa kufuata utaratibu ulioanishwa katika Kifungu cha
38 (8) na (9) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori, kifungu hiki kinampa Mamlaka
Waziri kuongeza muda wa umiliki wa vitalu (Renew of hunting blocks). Kanuni ya
16 kanuni ndogo ya (1), (2), (3), (4), (5), (7), (8), (9) na (10) ya Kanuni za
Uwindaji wa Kitalii zinatoa utaratibu wa kufuatwa wakati wa kuongeza muda
wa umiliki wa vitalu kwa muhula mwingine wa uwindaji na utaratibu huo
umefuatwa.
Kwa kuzingatia utaratibu huo, wamiliki wa sasa wa
vitalu kama Kanuni zinavyoelekeza, waliwasilisha maombi yao Wizarani. Idara ya
Wanyamapori ilipitia maombi hayo na kuwasilisha kwenye Kamati ya Ushauri ya
Ugawaji wa Vitalu vya Uwindaji. Kamati hiyo ilipitia maombi hayo tarehe 26 hadi
27 Julai 2016 na tarehe 13 Januari 2017. Hivyo, baada ya Kamati kukamilisha
taratibu zote na kujiridhisha iliwasilisha ushauri wake kwa Mhe. Waziri.
Kifungu cha 38 (6) cha Sheria ya Kuhifadhi
Wanyamapori alichokitaja mwandishi wa gazeti hilo, kinaeleza utaratibu wa
ugawaji wa vitalu kwa waombaji wapya na siyo kwa wale wanaoomba kuendelea na
umiliki wa vitalu kwa msimu mwingine (renewal).
Uongezaji wa muda wa umiliki wa vitalu vya uwindaji
ulifuata Sheria, Kanuni na Taratibu, Hivyo tunawoamba wananchi wapuuze habari
hiyo kwani mwandishi alikusudia kuupotosha umma kwa kunukuu na kutafsiri
vifungu vya Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori isivyo sahihi.
Imetolewa na,
KATIBU MKUU
29 Januari, 2017