*TUTAENDELEA KUTENGENEZA SERA RAFIKI KUVUTIA UWEKEZAJI SEKTA YA MAFUTA NA GESI ASILIA-KAMISHNA SHIRIMA*
📌 *Asema Sekta ya Mafuta nchini imeimarika*
📌 *Ataja miradi ya kimkakati ujenzi wa mabomba ya gesi na mafuta*
Kamishna wa Petroli, Goodluck Shirima amesema kuwa, Tanzania imejipanga vyema kutengeneza sera rafiki zitakazozidi kuvutia uwekezaji kwenye sekta ya Mafuta na Gesi Asilia ambazo zitawezesha pia kupata mitaji ya kuendesha Sekta kwa ufanisi.
Kamishna Shirima amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati wa Kongamano na Maonesho ya Petroli ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAPCE’25) linalofanyika kwa Siku Tatu jijini Dar es Salaam.
“ Katika Mkutano wa EAPCE’25 tumejadili kuhusu umuhimu wa kuwa na mikataba ambayo ina uwazi, inayotabirika na yenye manufaa kwa nchi na kwa wawekezaji. Mabenki na taasisi za kifedha zipo tayari na zina hamu ya kufadhili miradi hii, sisi kama Serikali jukumu letu ni kutengeneza mazingira sahihi kupitia sera zetu na sheria.” Amesema ShirimaKuhusu Sekta ya Mafuta nchini, amesema kuwa imeimarika kwani mafuta yapo na yanapatikana kwa bei himilivu na kwamba sasa bei ya kushushia mafuta kwenye bandari zote zinafanana kwa lengo la kupunguza gharama kwa Watanzania.
Kuhusu mkondo wa kati wa petroli, Shirima amesema kuwa Serikali inaendelea kuwa na miradi ya kimkakati ya usafirishaji mafuta na gesi ambapo Serikali ya Tanzania na Zambia ziko kwenye mazungumzo ili kujenga bomba jipya la kusafirisha mafuta ambalo litasaidia kusambaza mafuta pia katika sehemu ambazo linapita kama vile Morogoro, Njombe na Mbeya.
Ameongeza kuwa, kuna mazungumzo yanaendelea na Serikali ya Uganda ili kujenga bomba la kusafirisha mafuta safi kutoka Tanzania kwenda Uganda na pia ujenzi wa bomba la gesi kwenda nchini humo ambalo pia litasambaza gesi sehemu ambazo linapita.Amesema kuwa chini ya uongozi madhubuti wa Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko miradi hiyo itatekelezwa kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo, Mhandisi Joyce Kisamo kutoka Wizara ya Nishati amesema kuwa mkutano huo ambao umeendeshwa kwa mafanikio umehudhuriwa na Viongozi wa Ngazi mbalimbali kuanzia ngazi ya Mawaziri, Makatibu pamoja na Wataalam wabobezi wa Sekta kutoka nchi 6 za Afrika Mashariki.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni