ALIYEKUWA JIPU KWA MAGUFULI AULA SHAVU KUBWA AFRIKA,NI OMBENI SEFUE,SOMA HAPO KUJUA
Mwanadiplomasia mahiri wa Tanzania aliyepata pia
kuwa Katibu Kiongozi-Ikulu, Balozi Ombeni Sefue ameteuliwa kuwa Mtanzania wa
kwanza kuingia katika Jopo la Watu Mashuhuri katika Mpango wa Afrika
Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM).
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa APRM tawi la
Tanzania, Rehema Twalib anayehudhuria mikutano ya Umoja wa Afrika na APRM mjini
Addis Ababa, Ethiopia, Balozi Sefue ameidhinishwa kwenye kikao cha juu ya Wakuu
wa Nchi za Umoja wa Afrika ambao ni wanachama wa APRM kilichofanyika juzi
Jumamosi mchana.
“Haikuwa kazi rahisi kupata nafasi hii.
Nchi nyingi za Afrika zilileta majina ya watu wao mashuhuri ili kuingia katika
jopo hili muhimu. Balozi Sefue licha ya kuwa na utumishi uliotukuka kama
mwanadiplomasia mkongwe pia aliungwa mkono kwa nguvu zote na Serikali ya Awamu
ya Tano ya Tanzania,” alisema Katibu Mtendaji huyo.
APRM ni Mpango wa Afrika uliobuniwa na Wakuu wa
Umoja wa Afrika kwa lengo la kuwa na chombo kitakachosaidia kuhimiza nchi
wanachama kuenzi utawala bora na utoaji wa huduma bora za kiuchumi, biashara na
za kujamii kwa wananchi wao kupitia mfumo wa kujitathmini zenyewe na kukosoana.
Kwa mujibu wa tovuti ya APRM, Jopo la Watu Mashuhuri
ni chombo cha juu cha kuwashauri Wakuu wa Nchi Wanachama wa APRM katika
uendeshaji wa Mpango huo na husimamia mchakato mzima wa kujitathmini.
Wajumbe wa jopo hilo ambao hudumu hadi miaka minne
hupendekezwa na nchi zao na baada ya mchakato mrefu wenye ushindani majina ya
waliokidhi vigezo huwasilishwa na kuidhinishwa na na kikao cha juu katika
APRM-Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Tanzania ni miongoni mwa wanachama 35 kati ya nchi
54 wa Nchi za AU zilizojiunga na APRM na ilijiunga rasmi na Mpango huo tangu
mwaka 2004.Tayari Tanzania ilishafanyiwa tathmini ya kwanza ya utawala bora na
inaendelea kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa.
Katika mkutano huo Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi za
APRM Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aliwapongeza wajumbe wa jopo hilo na kuwata
kushiriki vyema katika kuihuisha APRM na kuwa chombo chenye thamani kubwa kwa
Afrika kama walivyotarajia waasisi wake akina Thabo Mbeki, Olusegun Obasanjo,
Benjamin Mkapa na wengine.
Balozi Sefue ataungana na wajumbe wengine wapya
ambao ni pamoja na Prof. Ibrahim Agboola Gambari (Nigeria), Balozi Mona Omar
Attia (Misri) Bi. Fatma Zohra Karadia (Algeria), Askofu Don Dinis Salomão
Sengulane (Msumbiji) na Prof. Augustin Loada (Burkina Faso). Wajumbe wa zamani
wanaoendelea ni pamoja na Prof. Youssouf Khayal (Chad) ambaye kwa sasa
atakuwa Mwenyekiti wa Jopo hilo na Brigitte Mabandla (Afrika Kusini) ambaye
atakuwa Makamu Mwenyekiti.
Mkutano huo pia ulijadili Ripoti za tathmini za nchi
katika maeneo anuai ya utawala bora kwa nchi za Kenya (ikiwa ni ripoti ya pili
kuwasilishwa), Sudan, Chad, Senegal, Djibouti pamoja na ripoti ya utekelezaji
ya Zambia.