Zinazobamba

Shein aendeleza ‘mchecheto’ Zanzibar,

DK. Ali Mohamed Shein Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, amesema ataendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuimarisha hali ya amani na utulivu wa kudumu visiwani Zanzibar, anaandika Wolfram mwalongo.
Dk. Shein ametoa kauli hiyo katika sherehe za kuadhimisha miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika katika uwanja wa Amani, katika hali inayoashiria kuendelea kuumizwa kichwa na sintofahamu ya kisiasa iliyopo visiwani humo.
Amesema wajibu wa kudumisha amani ni wa viongozi na wananchi wote bila kujali itikadi za vyama vyao.
“Napongeza ustahimilivu wa Wazanzibar hususan katika kipindi cha uchaguzi wa marudio wa tarehe 20 Machi 2016 ambao mimi nilitangazwa mshindi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar – ZEC chini ya mwenyekiti wake Jecha Salim Jecha,” amesema.
Kauli ya Dk. Shein kuwa atanendelea kushirikiana na Serikali ya Muungano ili kuimarisha amani visiwani humo inakuja ikiwa ni siku moja tu tangu Tundu Lissu, Mbunge na Mwanasheria Mkuu wa Chadema ahutubie wananchi visiwani Zanzibar na kusema majeshi ya Tanganyika yanaendelea kuikalia kijeshi Zanzibar na kufanya vitendo viovu ukiwemo uvunjifu wa haki za binadamu.
Lissu alikuwa akizungumza na wananchi katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani, Unguja ambapo alisema kuwa kauli ya Rais John Magufuli kuwa Dk. Shein awe anampigia simu ikiwa kuna mtu analeta ‘fyoko fyoko’ visiwani Zanzibar zinathibitisha kuwa Dk. Shein si chochote si kitu kwa Rais Magufuli.
Katika hotuba yake ya leo, Dk. Shein amekiri kuwepo kwa udhalilishaji visiwani humo huku serikali yake inaandaa mpango maalumu kwaajili ya kukabiliana na vitendo hivyo.
Amewatangazia neema wafanyakazi kwa kusema “Kuanzia April mwaka huu kiwango cha chini cha mshahara kitakuwa Sh. 300,000/= (laki tatu), badala ya Sh.150,000/= (laki moja na elfu hamsini) ambayo inalipwa kwa sasa.