RAIS MAGUFULI AANZA KUYAKOLOMEA MAGAZETI, AAPA KUYAFUNGIA MAGAZETI MAWILI,SOMA HAPO KUJUA
Rais wa Jamhri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli, leo tarehe 13 Januari, 2017 ameyaonya magazeti mawili
yanayoandika habari za uchochezi na kupotosha wananchi kwa kuwa vinahatarisha
amani ya nchini.
Rais Magufuli ametoa onyo hilo wakati akikagua na
kufungua Kiwanda cha Jambo cha kuzalisha vinywaji baridi mkoani Shinyanga.
Rais Magufuli amesema Serikali haitayavumilia
magazeti hayo mawili kwa kuandika habari za uchochezi ambazo zinaweza
kuhatarisha amani ya nchi kama ilivyotokea katika nchini ya Rwanda na kupelekea
mauaji ya kimbari nchini humo.
''Serikali ya kutumbua majipu haiwezi
kuacha kutumbua magazeti yanayofanya mambo ya uchochezi hatuwezi kuiacha
Tanzania ikawa dampo la eneo la kuweka maneno ya uchochezi chini ya utawala
wangu hilo halitakuwepo kuna magazeti mawili tu kila ukisoma wao ni kuchochea
tu ikizungumzwa habari hii wao wanageuza hii nasema na nataka wanisikie siku
zao zimeshafika kama wanasikia wasikie wasiposikia wasisikie lakini magazeti
mengine na vyombo vyote vingine vinatoa uchambuzi mzuri sana''.
Rais Magufuli amesema Serikali yake haiwezi
kuvumilia kuona amani ya nchi inahatarishwa na magazeti mawili kwani amani ndio
chimbuko la maendeleo ya taifa lolote duniani.
Amesema bila kuwepo kwa amani hakuna mwekezaji
atakayeweza kuja kuwekeza nchi, hata wawekezaji wa ndani watashindwa na hivyo
kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Rais Magufuli amesema uwepo wa amani nchini ndio
uliowezesha wawekezaji wa Kiwanda cha Fresho cha kutengenezea mifuko ya kubebea
bidhaa za chakula nchini na kiwanda cha Jambo cha kuzalisha vinywaji baridi
mkoani Shinyanga kujengwa mkoani hapo kwani bila amani visingeweza kujengwa.
Aidha ameitaka Benki ya Uwekezaji Nchini TIB na
Taasisi nyingine za fedha kutoa mikopo kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika
viwanda badala ya kuwakopesha wanasiasa ambao hutumia fedha wanazokopa kwa
matumizi yasiyowanufaisha watanzania waliowengi
Rais Magufuli ameupongeza uongozi wa mkoa wa
Shinyanga kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya kutaka Tanzania
ya viwanda kwa kujenga viwanda vingi mkoani humo ikiwa ni pamoja na viwanda
hivyo viwili alivyovizindua katika siku yake ya mwisho ya ziara mkoani
Shinyanga.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu
Shinyanga
13 Januari 2017.