Mganga Auawa Kwa Kuchomwa Visu........Kisa ni Kuwatapeli Watu Kwamba Atawapa Utajiri
Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la DOTTO MWAIPOPO
mkazi wa Kafundo – Ipinda wilayani Kyela Mbeya ameuawa kwa kuchomwa kisu ubavu
wa kulia na BONIPHACE KISWAGA Mfanyabiashara na Mkazi Chaugingi Mkoani Njombe
kwa madai ya kufanya utapeli.
Taarifa ya Polisi Mkoa wa Mbeya imesema tukio hilo
limetokea mnamo tarehe 11.01.2017 majira ya saa 4 usiku katika Kitongoji cha
Ipinda – Chini, Kijiji na Kata ya Ipinda, Tarafa ya Tembela, Wilaya ya Kyela,
Mkoa wa Mbeya.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni kulipiza
kisasi baada ya marehemu kuwatapeli watuhumiwa pesa ambazo kiasi halisi bado
hakijafahamika kwa madai kuwa yeye ni mganga wa kienyeji na atawasaidia kuwa
matajiri.
Aidha katika tukio hilo mtuhumiwa huyo BONIPHACE
KISWAGA alijeruhiwa kwa kupigwa na wananchi na amelazwa katika Hospitali ya
Wilaya ya Kyela kwa matibabu. Watuhumiwa wengine wawili ambao walikuwa pamoja
na mtuhumiwa aliyekamatwa walikimbia na msako mkali unaendelea.