LOWASSA AKASIRIKA,AYASEMA MAGAZETI YANAYOMCHAFUA,SOMA HAPO KUJUA
Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu
ya Chadema, Edward Lowassa, amesema kasi ya kuimarika kwa umoja na mshikamano
miongoni mwa vyama vya upinzani nchini, kunaitia kiwewe CCM kiasi cha kuanzisha
mbinu chafu za kisiasa.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini Kahama katika Hoteli
ya Gaprina ambapo alifikia kabla ya kuanza safari ya kuelekea mkoani Kagera
katika ziara ya kuimarisha chama chake.
Alisema kuimarika kwa mshikamano huo chini ya
mwavuli wa Vyama Vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni hatua
kubwa katika kuelekea kuing’oa CCM.
“Wameanza mbinu zao za kutaka kutuondoa
katika umoja wetu, wameanza kuwalisha viongozi wetu maneno, mfano gazeti
(nalitaja jina) la leo (jana) wamenilisha maneno ya kwamba eti nimeitabiria CCM
ushindi katika uchaguzi mdogo wa udiwani kule Arumeru.
“… mambo ya ajabu kabisa hili
gazeti linaishi kwa kodi zetu sisi wananchi leo linaamua kutumika kuvunja
demokrasia inasikitisha sana.
“Wanaandika uongo mchana kweupe kuwa
nilikuwa katika kampeni kwenye kitongoji Ematasia..mimi sikwenda huko..lakini
mbinu zao hizi wananchi wameshazijua na hawako tayari kuona hamu yao ya kupata
mabadiliko inapotea,” alisisitiza.
Wakati huo huo mamia ya wakaazi wa mji wa Kahama
waliizingira Hoteli ya Gaprina alikofikia Lowassa, wakiwa na nia ya kutaka
kumwona.
Akiwa njiani kuelekea Bukoba, Lowassa na msafara
wake alipata nafasi ya kusalimiana na wananchi katika mnada wa Lusaunga
wilayani Biharamlo, ambako wananchi hao walimwambia kuwa hali yao ya maisha ni
ngumu pamoja na hali mbaya ya ukame inayowakabili.
Hata hivyo Lowassa hakutoa kauli yoyote kwao zaidi
ya kusema kwa sasa mikutano ya hadhara imepigwa marufuku na asingependa kuvuja
sheria kwa kile alichodai amri kandamizi.