RAIS MAGUFULI AWATOA HOFU WATANZANIA KUHUSU UPANDAJI WA UMEME,SOMA HAPO KUJUA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amewahakikishia Watanzania kuwa licha ya Mamlaka ya
udhibiti wa huduma za Nishati, Maji na Mafuta (EWURA) kuridhia ombi la TANESCO
la kupandisha bei ya umeme kuanzia Januari mosi,2017 bei ya umeme haitapanda.
Rais Dkt. Magufuli amezungumza hayo leo Jumapili ya
Januari Mosi, 2016 wakati wa Ibada katika Kanisa la Bikira Maria Mama
Mwenye Huruma,Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la Bukoba anapoanza rasmi ziara ya
kikazi ya siku mbili Mkoani Kagera.
Rais Magufuli ameshangazwa na kitendo cha watendaji
waliopandisha bei ya umeme bila hata ya kushauriana na yeye, Makamu wa
Rais,Waziri Mkuu au Waziri mwenye dhamana ya Nishati na Madini Prof Sospeter
Muhongo na hivyo kumshukuru Waziri Muhongo kwa kutengua maamuzi hayo.
''Ninamshukuru sana Waziri wa Nishati na
Madini kwa maamuzi ya kusitisha hayo kwa hiyo umeme hakuna kupanda
bei,haiwezekani unapanga mikakati ya kujenga viwanda na hasa katika mikakati
mikubwa ya nchi ya kusambaza umeme mpaka vijijini,na umeme huu unaenda kwa watu
masikini walioumbwa kwa mfano wa Mungu halafu mtu pekee kwa sababu ya cheo
chake anapandisha bei,hili haliwezekani'' Alisema Rais
Dkt. Magufuli.'
Aidha, Rais Dkt Magufuli ameendelea kuwataka
watanzania katika mwaka huu mpya 2017 kuendelea kufanya kazi kwa bidii kama
maandiko matakatifu yanavyoelekeza kuwa asiyefanya kazi na asile badala ya
kulalamika kuwa fedha zimepotea.
Kwa upande wake,Askofu Msaidizi Jimbo Katoliki la
Bukoba,Askofu Methodius Kilaini,akitoa mahubiri kwa waumini waliohudhuria ibada
hiyo amempongeza Rais Dkt Magufuli kwa uongozi wake imara,huku akisema kupungua
kwa urasimu katika ofisi za umma kunatokana na utendaji kuongezeka na
kuwataka wana Kagera na Watanzania kwa ujumla kumuunga mkono Rais Magufuli kwa
kufanya kazi kwa bidii na uaminifu.
Mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na
Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba,Askofu Desderius Rwoma,Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli aliwatakia heri ya mwaka mpya waumini wa
kanisa hilo na watanzania kwa ujumla.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kagera.
01 Januari, 2017