LOWASSA AMPA TANO TRUMP WA MAREKANI,ADAI YEYE SAHIVI ANAFANYA SIASA ZA KIMATAIFA,SOMA HAPO KUJUA
WAZIRI Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amewapongeza
raia wa Marekani kwa kumchagua Donald Trump kuwa rais mpya wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa Lowassa, Trump atakuwa rais mwenye
kufanya uamuzi mgumu kwa kuwa ni shupavu na ana uwezo.
Trump ambaye ni Rais Mteule wa Marekani,
alichaguliwa kuwa Rais mpya wa Marekani baada ya kumshinda mpinzani wake,
Hillary Clinton, mwishoni mwa mwaka jana.
Lowassa aliyasema hayo jana katika misa maalumu ya
shukrani ya mwaka mpya 2017 iliyoshirikisha madhehebu mawili ya Kanisa la
Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Monduli na Kanisa Katoliki,
wilayani Monduli, Mkoa wa Arusha.
Ibada hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali
wakiwamo wa Serikali na wa vyama vya siasa, wakiwamo Meya wa Jiji la Arusha,
Calist Lazaro ambaye pia ni Katibu wa Chadema, Mkoa wa Arusha.
“Wamarekani hawakufanya makosa kumchagua Trump kwani
anaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuongoza Taifa hilo tajiri duniani ambalo
linategemewa na mataifa mengine.
“Dunia imebadilika, amechaguliwa rais mmoja huko
Marekani ambaye ni mwamba kweli kweli.
“Hatuwezi kumtabiri mambo yake yatakavyokuwa, lakini
inabidi kila mtu afanye kazi kwa bidii na kwa maarifa kwa sababu huyo hakubali
upuuzi wowote,”alisema Lowassa.
Lowassa ambaye pia aliwahi kuwa Mbunge wa Monduli
kwa miaka 20, aliwataka wananchi kufanya kazi kwa bidii na kuacha kulalamika
kwani hiyo ndiyo njia iliyo sahihi ya kuweza kuondokana na umasikini.
“Mwaka jana, tarehe kama hii, tulimuaga Mbunge
Julius Kalanga na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Isack Joseph,
nikawaambia nawatakia heri wachape kazi vizuri, naona wamefanya vizuri au
siyo?alihoji Lowassa.
Akizungumzia upande wake, Lowassa alisema hivi sasa
anafanya siasa za kimataifa tofauti na siasa alizokuwa akifanya kipindi
kilichopita.
“Mimi sitaki kusema sana maana watasema napiga
siasa. Siku hizi napiga siasa za kimataifa, naomba niwatakie heri ya mwaka mpya
na kila mtakachoshika, Mungu akibariki kiwe dhahabu,”alisema