RAIS MAGUFULI AMFUKUZA KAZI BOSI WA TANESCO,SOMA HAPO KUJUA
MHANDISI Felchesmi Mramba aliyekuwa Mkurugenzi
Mtendaji wa Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) amekuwa mtumishi wa kwanza wa
serikali kutimuliwa kazi na Rais John Magufuli kwa mwaka 2017, anaandika Charles William.
Mramba ameng’olewa ikiwa ni siku moja tu tangu Mamlaka ya Uthibiti
wa Huduma ya Nishati na Maji (EWURA) kutangaza kuwa bei ya umeme itapanda kwa
asilimia tano, kuanzia Januari Mosi mwaka huu kufuatia maombi ya Tanesco
iliyotaka kupandisha bei ya nishati hiyo kwa angalau asilimia 18.
Hata hivyo masaa machache baada ya taarifa hiyo ya
Ewura, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini alitangaza kuzuia
kupanda kwa bei hiyo, huku akiishushia tuhuma menejimenti ya Tanesco kuwa
inapandisha bei ili ipate fedha za kugawana kama sehwmu ya marupurupu yao.
Taarifa iliyotolewa jioni hii na Gerson Msigwa,
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu imesema kuwa Rais Magufuli ametengua
uteuzi wa Mramba huku akimteua Dk. Tito Esau Mwinuka ili kukaimu nafasi hiyo.
Rais Magufuli amefanya maamuzi hayo akiwa ziarani
mkoani Kagera ambapo kabla ya kutangazwa rasmi kwa uamuzi huo, asubuhi ya leo
alipohudhuria misa katika ibada iliyofanyika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la
Bukoba alinukuliwa akisema kitendo cha kupandisha umeme hakikubaliki kwani
serikali yake ipo katika juhudi za kuanzisha uchumi wa viwanda na kusambaza
umeme vijijini.
“Ndiyo maana tunasema muendelee kutuombea kwani
majipu bado yapo na nitaendelea kuyatumbua,” alisema Rais Magufuli.