RAIS MAGUFULI AMALIZA ZIARA YAKE MKOANI KAGERA,SOMAHAPO KUJUA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli leo Jumatatu Januari mbili, 2017 amemaliza ziara yake ya
siku mbili Mkoani Kagera kwa kuwatembelea baadhi ya wananchi walioathiriwa na
tetemeko la ardhi pamoja na kukagua baadhi ya miundo mbinu iliyoathiriwa na
tetemeko hilo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa majengo ya shule ya
sekondari ya Ihungo Omumwani iliyobomolewa na tetemeko la ardhi la
Septemba 10,2016.
Mara baada ya ukaguzi huo Rais Dkt Magufuli
akazungumza na wananchi wa Mkoa huo wa Kagera katika viwanja vya Shule ya
Sekondari ya Ihungo na kuagiza kuvunjwa kwa kamati ya maafa ya Mkoa huo
iliyokuwa ikiratibu utoaji wa misaaada na kufanya tathmini ya athari ya
tetemeko hilo.
”Kila kitu huwa kina mwanzo na mwisho wake ukiwa na
harusi huwa kuna kamati ya harusi,ukishamaliza kufunga ndoa kamati ya harusi
huwa inavunjwa,na ukiwa kwenye msiba huwa kuna kamati ya msiba na msiba
mkishazika kamati ya mazishi huvunjwa,kamati ya maafa ya Kagera huu ni mwezi wa
tano na inawezekana hata kwenye kamati huwa wanalipana posho,sasa nataka hii
kamati nayo iishe,yalishapita yamepita”
Aidha Dkt Magufuli amewataka wote walioahidi kuchangia
katika kamati ya tetemeko la ardhi ya mkoa wa Kagera ambao bado hawajatekeleza
ahadi zao ambazo ni jumla ya shilingi bilioni nne nukta tano wakamilishe ahadi
hizo ili ziweze kumalizia miundombinu ya Serikali iliyoathiriwa na tetemeko
hilo.
Ameongeza kuwa wale wote wanaoendelea kuguswa
kusaidia wapeleke michango yao moja kwa moja kwa wananchi badala ya kuipeleka
serikalini kwa kuwa hakuna mchango mwingine utakaopokelewa katika Ofisi ya
Waziri Mkuu.
Pia Rais Dkt Magufuli ameagiza shule ya Sekondari ya
Omumwani iliyokuwa inamilikiwa na Jumuia ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi CCM
imilikiwe na Serikali kutaka wanafunzi wote wanaosoma katika shule hiyo
kutolipa ada kama zilivyo shule nyingine za serikali.
Dkt Magufuli ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera
kupunguza utitiri wa kodi katika zao la kahawa ili bei ya zao hilo ipande na
kuwanufaisha wakulima
Balozi wa Uingereza hapa Nchini Bi Sarah Cooke
ambaye nchi yake imechangia kiasi cha shilingi bilioni sita kwa ajili ya ujenzi
wa shule ya Sekondari ya Ihungo, amempongeza Rais Dkt Magufuli na serikali yake
kwa jitihada za kupambana na rushwa suala ambalo nchi yake ya Uingereza inalipa
kipaumbele sambamba na kutoa elimu bila malipo jambo linalowawezesha watoto
wengi wa kitanzania kupata elimu bure
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kagera.
02 Januari, 2017