RAIS MAGUFULI AKASIRIKA,NI KUHUSU WANASIASA WANASEMA KUNA NJAA,SOMA HAPO KUJUA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli, leo tarehe 11 Januari, 2017 ameanza ziara ya siku mbili mkoani
Simiyu kwa kuwataka wananchi wa mkoa huo na Tanzania kwa ujumla kuwapuuza
watu wanaoendesha siasa alizozitaja kupitwa na wakati kwa kutumia baadhi ya
vyombo vya habari kutangaza kuwa Tanzania inakabiliwa na njaa badala ya
kuwahamasisha wananchi kufanya kazi
Dakta Magufuli amesema hayo wakati akizungumza na
wananchi katika uwanja wa Shule ya Msingi Somanda mara baada ya kuweka jiwe la
Msingi katika Hospitali ya Mkoa wa Simiyu na kufungua barabara ya Lamadi
hadi Bariadi yenye urefu wa kilomita 71.8 iliyogharimu zaidi ya shilingi
Bilioni 90.
Amesema kumekuwepo na baadhi ya wanasiasa na
wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiwahamisisha wananchi na kutumia baadhi ya
vyombo vya habari kutangaza baa la njaa wakati wanasiasa hao hao ndio
waliopitisha Bungeni kutaka nchi iuze chakula nje ya nchi na sasa hao hao
wanatangaza baa la njaa.
'' Baadhi ya wanasisa walizungumza
Bungeni kutaka wananchi waruhusiwe kuuza chakula nje ya nchi kwa kuwa kuna
chakula cha kutosha leo hii hao hao wanatumia baadhi ya vyombo vya habari
kutanga baa la njaa''
Akizungumzia gharama za ujenzi wa Hospitali ya
mkoa wa Simiyu, Rais Magufuli ameutaka uongozi wa mkoa wa Simiyu, Wizara ya
Ujenzi na Wakala wa majengo nchini TBA kukaa na kurejea gharama za ujenzi wa
Hospitali hiyo wa Shilingi Bilioni 46 kuwa hauendani na hali halisi ya aina ya
jengo linalotakiwa kujengwa.Rais Magufuli ametoa Shilingi bilioni 10 ili
kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo.
''Haiwezekani majengo ya ghorofa ishirini
lijengwe kwa shilingi Bilioni Kumi wakati jengo la ghorofa moja moja lijengwe
kwa gharama ya shilingi Bilioni 46''
Rais Magufuli pia ameutaka uongozi wa mkoa wa Simiyu
kuendelea na ujenzi wa mradi wa tenki la maji katika mlima Ngasamo ili wananchi
wa mkoa wa Simiyu ikiwemo wilaya ya Bariadi kupata huduma ya maji badala ya
kukwama kutokana na mwekezaji mmoja kutaka kuchimba madini ya Nikeli katika
mlima huo.
Amesema haiwezekani wananchi zaidi ya milioni moja
wakose maji kutokana na mwekezaji mmoja ni kukosa muelekeo na kumkosea Mwenyezi
Mungu kitu kisichokubalika hivyo Waziri wa Nishati na Madini afute leseni ya
mwekezaji huyo ili wananchi wa Simiyu wapate huduma ya maji.
Rais Magufuli amewataka wananchi wa Mkoa wa Simiyu
na Watanzania kwa ujumla kutumia mvua chache zinazonyesha kulima mazao
yanayostahamili ukame kama vile Mtama,viazi na Uwele ili kuweza kujikimu kwa
chakula badala ya kutegemea chakula cha msaada kutoka Serikali.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Simiyu
11 Januari, 2017