NEC YAZIJIBU TUHUMA ZA CHAMA CHA ACT-WAZALENDO,SOMA HAPO KUJUA
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekishauri Chama
cha ACT – Wazalendo na Vyama vingine vyenye wagombea wa Ubunge katika Uchaguzi
Mdogo wa Jimbo la Dimani na Udiwani katika Kata Ishirini (20) za Tanzania Bara
,kuwasilisha malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi kwenye Kamati za
Maadili zilizo katika maeneo yao.
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es
salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Kailima
Ramadhan amesema NEC imepata taarifa kupitia Vyombo mbalimbali juu ya
malalamiko ya Chama Cha ACT-Wazalendo kuvilalamikia Vyombo vya Dola pamoja na
Watendaji wa Umma kufanya vitendo vyenye muelekeo wa kukipendelea Chama Cha
Mapinduzi (CCM).
Bw. Kailima amesema taarifa ya Chama hicho
iliyotolewa kwenye Vyombo vya Habari Januari, 12 2017, imeeleza kuwa Watendaji
wa Halmashauri ya Geita waliwakusanya Wazee katika Kata ya Nkoma waje na
Vitambulisho vyao vya kupigia Kura kwa lengo la kuwapatia huduma ya afya bure
jambo linalolalamikiwa na ACT- Wazalendo kwa madai kwamba Watendaji hao wana
lengo la kuwahadaa Wazee hao ili wakipigie Kura Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, amesema katika malalamiko yake Chama cha ACT
Wazalendo kimeibua tuhuma za wananchi kupokwa kadi za kupigia Kura ili wasiweze
kushiriki katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Januari 22, 2017.
Mkurugenzi Kailima amesisitiza kuwa ni kosa chini ya
kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 100
cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 mtu kumiliki kadi ya
kupigia kura isiyokuwa yake.
“Natoa wito kwa wananchi wote kwamba, ni kosa chini
ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha
100 cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 mtu yeyote
kumiliki kadi ya kupigia kura isiyokuwa yake” Amesema.
Amefafanua kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa
kuzingatia sehemu ya 5.4 ya Maadili ya Uchaguzi inavikumbusha Vyama vya Siasa
kuwa iwapo vitakuwa na malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi katika
Uchaguzi Mdogo wa Udiwani viwasilishe malalamiko hayo kwenye Kamati ya Maadili
ngazi ya Kata ndani ya saa 72 tangu kutokea kwa tukio linalolalamikiwa.
“ Sehemu ya 5.4 ya Maadili ya Uchaguzi yayosainiwa
na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Serikali na Vyama Vya Siasa inaeleza wazi muda wa
kuwasilisha malalamiko kwa kuvitaka vyama au wahusika wenye malalamiko yoyote
kuyawasilisha kwa maandishi kwenye Kamati ya Maadili ya Uchaguzi ya ngazi
husika ndani ya saa 72 tangu kutokea kwa tukio” Amesisitiza Kailima.
Amesisitiza kuwa iwapo Chama cha Siasa au Mgombea
hataridhika na maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Kata, kwa kuzingatia
sehemu ya 5.7 (a) ya Maadili ya Uchaguzi anatakiwa awasilishe rufaa yake kwa
Msimamzi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo ndani ya saa 24 tangu maamuzi ya Kamati ya
Maadili ngazi ya kata kutolewa.
Aidha, Bw. Kailima amebainisha kuwa kama Chama cha
Siasa hakikuridhika na maamuzi ya Kamati ya Maadili ngazi ya Jimbo, bado kwa
kuzingatia sehemu ya 5.7 (b) na (c) kinayo fursa ya kuwasilisha Rufaa yake
katika Kamati ya Maadili ngazi ya Taifa au ngazi ya Rufaa ambayo ni Tume ya
Taifa ya Uchaguzi.
“ Tunavishauri Vyama vya Siasa na Wagombea
kuzingatia matakwa ya Maadili ya Uchaguzi katika kuwasilisha malalamiko yao ya
ukiukwaji wa maadili ya Uchaguzi, kwa mujibu wa sehemu ya 5.7(e) ya Maadili ya
Uchaguzi, pale ambapo Chama cha Siasa au Mgombea hakuridhika na maamuzi ya
Kamati ya Rufaa atakuwa na fursa ya kuwasilisha malamiko yake Mahakamani baada
ya Uchaguzi kwa mujibu wa Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Sheria ya
Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292”.
Amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi
inaendelea kuwasihi viongozi wa Vyama vya Siasa na Wadau wengine wa Uchaguzi
kuendelea na Kampeni za kistaarabu na kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili ya
Uchaguzi na kwamba inaendelea kufuatilia kwa karibu kila hatua ya Uchaguzi na
hasa Kampeni huku akisisitiza kuwa haitasita kuchukua hatua kwa mtu yeyote
atakayekiuka Sheria za Uchaguzi.