MAWAZIRI SABA WA MAGUFULI WAJITOSA KUPAMBANA NA UVUVI HARAMU,SOMA HAPO KUJUA
Naibu waziri Tamisemi selemani Jafo akizungumza na waandishi wa habari kulia waziri ofisi ya makamu wa rais muungano na mazingira mh January Makamba |
Kukithiri kwa uvuvi haramu hasa wa kutumia mabomu
kumesababisha mawaziri wa wizara saba kukutana ghafla ili kujadiliana namna ya
kukabiliana na tatizo hilo.
Mawaziri hao ni January Makamba (Muungano na
Mazingira ), Dk Charles Tizeba (Kilimo na Mifugo na Uvuvi), Dk Hussein Mwinyi
(Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa) na Mwigulu Nchemba (Mambo ya Ndani ya Nchi).
Wengine ni Profesa Jumanne Maghembe (Maliasili na Utalii) na Seleman Jafo (Naibu
Waziri wa Tamisemi) wakati Wizara ya Uchukuzi iliwakilishwa na katibu mkuu, Dk
Leonard Chamulilo.
Akizungumza na wanahabari jana baada ya kikao hicho,
Makamba alisema lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadiliana namna ya kuchukua
hatua za kukabiliana na uvuvi huo.
Makamba ambaye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho,
alisema Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali za bahari na samaki, lakini
zinaathiriwa na uvuvi haramu.
“Tumejadiliana kwa kirefu na
tumetafakari hatua za kuchukua ili kukomesha tabia hii. Kikao kilikuwa cha
kazi, mikakati na mbinu za kukabiliana na watu wanaofanya uvuvi haramu,”
alisema Makamba.
Hata hivyo, hakuwa tayari kuzitaja hatua
walizokubaliana na mawaziri wenzake badala yake alisema taarifa kwa kina
itatolewa siku zijazo.
Kwa mujibu wa Makamba, baada ya miezi sita mawaziri hao watakutana na kupeana mrejesho wa kujua hatua walizokubaliana zimefanikiwa kwa kiwango gani.
Kwa mujibu wa Makamba, baada ya miezi sita mawaziri hao watakutana na kupeana mrejesho wa kujua hatua walizokubaliana zimefanikiwa kwa kiwango gani.
“Shughuli hii ni vita, lazima tupambane.
Nguvu ya Serikali iliyopo hapa (mawaziri) itawashukia wahusika pasipo kujua,” alisema
Makamba.
Dk Tizeba alisema mazingira ya bahari yanazidi kuharibika na kwamba asilimia 40 ya matumbawe ya samaki yameathiriwa na uvuvi huo.
“Lazima tuchukue hatua madhubuti
kukomesha uvuvi haramu. Tumejipangia hatua za muda mrefu na mfupi katika hili,”
alisema.
Waziri huyo aliongeza kuwa Tanzania ndiyo nchi
iliyobaki na aibu ya kuvua samaki kwa kutumia milipuko ya mabomu, jambo
linaloiletea sifa mbaya.
Nchemba alieleza kuwa kila Mtanzania ana wajibu wa
kushirikiana na Serikali kukomesha vitendo hivyo kwa kutoa taarifa kwenye
vyombo vya dola.
“Wafichueni wote wanaofanya vitendo hivi
na motisha ipo kwa mtoa taarifa,” alisema Nchemba.