AJALI MBAYA YATOKEA TENA MKOA WA SINGIDA,SOMA HAPO KUJUA
Matukio ya ajali za barabarani yameendelea kuutikisa
Mkoa wa Singida baada ya abiria 10 kupoteza maisha na wengine zaidi ya 30
kujeruhiwa ndani ya siku tisa.
Desemba 30, mwaka jana katika Kijiji cha Tumuli
Wilaya ya Iramba abiria watatu walikufa na wengine 25 kujeruhiwa na ajali
nyingine ilitokea Januari Mosi katika Kijiji cha Kintukuntu wilaya humo na kuua
abiria mmoja na kujeruhi watatu.
Ajali nyingine iliyohusisha bajaji ilitokea
jana Januari 7 katika Barabara ya Mwankoko na kumuua dereva na
abiria wawili.
Siku moja kabla ya tukio hilo, ajali ya basi la
Mohammed Trans lililokuwa linatokea Tanga kwenda Shinyanga ilisababisha vifo
vya abiria watatu na kujeruhi wengine watano wote wakiwa ni walimu.
Akitoa taarifa ya ajali ya basi la Mohammed Trans
jana, Kaimu Kamanda Polisi mkoani hapa, Mayala Towo alisema ilitokea Januari 6,
saa nne usiku katika Kijiji cha Mseko wilayani Iramba.
Kamanda huyo aliwataja waliofariki dunia kuwa ni
Mussa Rajabu (55), Farahan Manyama (34) na John Tungaraza (39) wote wakiwa ni
walimu, wakazi wa Geita.
Pia, alisema majeruhi ambao pia ni walimu wamelazwa
katika hospitali ya wilaya hiyo.
Kamanda huyo aliongeza kuwa walimu hao walikuwa
wametokea kwenye Chuo cha Eckenford mkoani Tanga walikokuwa wakichukua mafunzo
mbalimbali. Alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva.
Towo alisema basi hilo lenye namba za usajili T 786
AWJ aina ya Scania lilikuwa linaendeshwa na Jovin Jackson (38), mkazi wa
Shinyanga liligonga kwa nyuma lori lenye namba B.6705A lililokuwa likivuta tela
B.0568A lililokuwa likienda Burundi.
Akifafanua, alisema dereva wa basi alitaka kulipitia
lori hilo, lakini alipogundua hataweza aliamua kurudi ghafla kushoto na mwendo
kasi aliokuwa nao alijikuta analigonga lori hilo kwa nyuma.
Towo alisema baada ya kusababisha ajali hiyo dereva
alitoroka na kukimbilia kusikojulikana. Juhudi zinaendelea kumsaka ili
afikishwe mahakamani.