BALAA LA NJAA LAITESA TAIFA,WANANCHI WAANDAMANA NA KUMVAA MKUU WA MKOA,SOMA HAPO KUJUA
Wakazi zaidi ya 300 wa Kata ya Mwagi wakiongozwa na
mbunge wao wa Sumve, Richard Ndassa wamepokea msafara wa Mkuu wa Mkoa wa
Mwanza, John Mongella kwa mabua ya mahindi mikononi mwao, kuashiria namna zao
hilo lilivyoathiriwa na ukame.
Mongella ambaye alikuwa ameambatana na Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, wakati wa ziara yake kukagua maendeleo ya
kilimo wilayani hapa, alikutana na hali hiyo katika Kijiji cha Mwabilanda
wakati akitokea Kijiji cha Manawa kukagua mashamba ya pamba.
Wakazi hao walisema wametekeleza wajibu wao, lakini
ukame umevuruga malengo yao huku wakiomba msaada wapelekewe chakula haraka.
Awali, akiwa Kijiji cha Manawa wakazi wake walisimama
barabarani kwa lengo la kutaka wapatiwe ufumbuzi wa namna Serikali
ilivyojipanga kuwanusuru na njaa iliyosababishwa na ukame.
“Kwa kweli hali yetu ya chakula
hapa kijijini ni mbaya. Mimi na umri wangu sijawahi kushuhudia hali kama hii
kwa zaidi ya miaka 40,” alisema mwenyekiti wa Serikali ya
kijiji hicho, Joseph Nkonoki.
Alifafanua kuwa baadhi ya wanaume wameanza
kutelekeza familia zao kutokana na kukosa namna ya kupata fedha kwa ajili ya
kununua chakula.
Akijibu malalamiko hayo Mongella alisema: “Timu
ya mkoa itakutana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya wiki ijayo ili
kuandaa taarifa ambayo baadaye Serikali itaifanyia kazi.Matokeo yake mtayaona
muda siyo mrefu.”
Mongella aliwashauri wakazi hao kulima mazao
yanayostahimili ukame katika kipindi hiki ambacho mvua zimekuwa za kusuasua.
Aliwataka kuwa na subira wakati Serikali ikiendelea
kujipanga, huku akisema ukame unachangiwa na mabadiliko ya hali ya hewa.
Pia, Mongella alimuagiza mkuu wa wilaya hiyo,
Mtemi Simeon kuwakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wananchi
watakaobainika kukata miti bila kibali chake.