MAKAMU WA RAIS AWAPA DARASA MAJAJI NA MAHAKIMU WANAWAKE NCHINI,SOMA HAPO KUJUA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Samia Suluhu Hassan amewaagiza majaji na mahakimu wanawake kote nchini
kupambana ipasavyo katika kukabiliana vitendo vya rushwa,unyanyasaji kijinsia na
rushwa ya ngono ili kusaidia wanawake kupata haki zao za msingi bila kubaguliwa
katika jamii.
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo
jijini Dar es Salaam wakati anafungua Mkutano Mkuu wa NANE wa Chama cha Majaji
na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA).
Makamu wa Rais pia ameonya kuhusu vitendo vya rushwa
ya ngono inayofanywa na baadhi ya watendaji wenye madaraka na kusema tabia hiyo
ni mbaya na lazima ikomeshwa mara moja katika jamii.
Amesema kuwa vitendo hivyo vya rushwa ya ngono huzuia
na kukwamisha juhudi za wanawake kufikia huduma za kijamii na za kiserikali
ipasavyo ikiwemo elimu, ajira na haki kwa ajili ya ustawi wa wanawake.
Aidha Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan
amekishukuru Chama cha Dunia cha Majaji Wanawake (IAWJ) kwa mchango na msaada
wake kwa TAWJA katika programu ya miaka mitatu ya kupambana na matumizi mabaya
ya madaraka na rushwa ya ngono.
Makamu wa Rais pia ameipongeza Wizara ya Katiba na
Sheria, Shirika la UN Women na wadau wengine wa TAWJA kwa kuunga mkono
mapambano ya aina zote za ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake na watoto
nchini.
Amesema elimu ya haki za Binadamu iliyotolewa na
Chama hicho imeleta badiliko kwa wengi kwa njia ya mafunzo na machapisho na
jitihada hivyo lazima ziongezwe ili huduma hiyo iweze kuwafikia wananchi wengi
zaidi kote nchini.
Amesisitiza wanachama wa Chama cha TAWJA waendelee
kutoa msaada katika kuwasaidia wanawake na watoto ambao wanakandamizwa kwa
kunyimwa haki zao katika jamii ili waweze kupata haki zao nchini.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mohamed Chande Othman amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa mkakati wa
uimarishaji wa shughuli za mahakama nchini unaendelea vyema lengo likiwa ni
kutenda haki kwa wananchi kote nchini bila ubaguzi.
Kauli mbiu ya Mkutano Mkuu wa NANE wa Chama cha
Majaji na Mahakimu Tanzania (TAWJA) “Kuongoza njia kufikia hitajio la
upatikanaji wa haki kwa wote na kwa wakati”.