LOWASSA ATEMA CHECHE ARUSHA ADAI MABADILIKO HAYAEPUKIKI,SOMA HAPO KUJUA
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema
mabadiliko makubwa ya kisiasa yanayotokea duniani katika kipindi hiki hayawezi
kuzuiliwa na mifumo iliyopo.
Akizungumza jana na mamia ya wananchi waliojitokeza
kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Mateves katika
Halmashauri ya Arusha Vijijini, Lowassa alisema nguvu kubwa ya mabadiliko
inayoonyeshwa na Chadema itawaletea wananchi maendeleo.
Lowassa ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema
alisema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, chama chake kilipata kura nyingi
kwenye maeneo mengi licha ya kutokuwa washindi na kwamba wamejipanga katika
uchaguzi wowote utakaofanyika kuhakikisha kinashinda kwa kishindo.
“Ninazindua kampeni za uchaguzi huu
mdogo nikiwa na imani kubwa kwa Chadema. Nina imani kuwa mgombea wa chama hiki
atatekeleza anayoyaahidi na kuondoa kero zenu na ndiyo maana Chadema inaungwa
mkono zaidi nchini,” alisema Lowassa.
Alisema katika mpango wa kukiimarisha chama hicho,
wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema wanazunguka nchi nzima kuanzia ngazi ya tawi
hadi Taifa.
Katika harakati za kuhakikisha kwamba upinzani
unaibuka na ushindi katika chaguzi ndogo zote zilizopangwa kufanyika Januari
22, Lowassa alisema leo atakuwa Zanzibar katika uzinduzi wa kampeni za mgombea
ubunge wa Dimani kwa tiketi ya CUF, Abdulrazaq Khatib Ramadhan na baada ya hapo
ataelekea Bukoba katika kampeni za Ukawa.
Uchaguzi wa Kata ya Mateves unafanyika baada ya
Mahakama kuagiza urudiwe kutokana na kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi ulipita
ambao mgombea wa CCM alitangazwa mshindi.