LOWASSANA SUMAYE WAMTEMBELEA LEMA GEREZANI,SOMAHAPO KUJUA
Mawaziri wakuu wa zamani ambao ni wajumbe wa
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa na
Fredrick Sumaye, jana wamemtembelea Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema katika
Gereza Kuu la Kisongo mjini Arusha.
Lowassa akiongozana na Meya wa Jiji la Arusha,
Calist Lazaro ambaye pia ni Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, ndiye aliyekuwa
wa kwanza kufika katika gereza hilo.
Calist alisema Lowassa alifika gerezani hapo saa
tano asubuhi huku Sumaye aliyeongozana na Naibu Meya wa Arusha, Viola Lazaro
akifika baadaye saa saba mchana.
Calist alisema Lowassa akizungumza na Lema,
alimwambia kuwa mahakama ndiyo chombo pekee kinachoaminiwa na wananchi, hivyo
kinapaswa kutenda haki kwa watu wote.
Alisema Lowassa aliridhishwa na afya ya Lema na
kumtaka awe mvumilivu, hasa katika kipindi hiki anachokabiliwa na kesi na
aliwataka wananchi wa Arusha Mjini kumwombea kiongozi huyo.
“Watanzania wana matumaini makubwa sana
na mahakama, wanaamini chombo hiki pekee ndicho kitakachowapa haki yao, hivyo
kwa mwaka 2017 mahakama itoe haki na kuendesha kesi bila upendeleo kwa sababu
ndiyo sauti ya wanyonge, nakutakia amani na mwaka mpya mwema,”
Calist alimnukuu Lowassa.
Kwa upande wake, Sumaye alisema kuwa alimtaka mbunge
huyo kuwa jasiri katika kipindi hiki kwa sababu suala linalomkabili litafika
mwisho.
“Mimi nilikuja tu kumsalimia, kumjulia
hali ya afya yake kwa sababu Lema tangu amekaa huku gerezani nilikuwa sijapata
nafasi ya kuja kumtembelea, kwa vile wakati huu niko katika maeneo haya ya
Kaskazini, nikasema nije kumsalimia, afya yake nzuri na nimemuona hana
wasiwasi, naona kabisa amekaa vizuri, ameelewa hiyo hali na amepokea, hana uso
wa kusononeka na hilo limenipa moyo.
“Nimemwachia ujumbe ‘just be strong’
(awe jasiri), haya yote yatapita muda wake ukifika, suala lake liko mahakamani
sio la kisiasa, hata kama lililomleta huku linahusiana na siasa, suala la
dhamana tunatarajia litafika mwisho wake, lakini nimemwambia hata kama dhamana
ikikosekana, bado kesi ya msingi itafika mwisho wake, asiwe na wasiwasi wala
hamaki, awe jasiri asikate tamaa,” alisema.
Desemba 11, mwaka jana, Katibu wa Taasisi za
Kiislamu Tanzania, Sheikh Issa Ponda, alimtembelea Lema katika gereza hilo na
alimtia moyo aendelee na mapambano na kumtaka asikate tamaa ya kupigania haki
za Watanzania.
Lema alikamatwa Novemba 2, mwaka jana akiwa nje ya
Viwanja vya Bunge mjini Dodoma na kufikishwa mahakamani Novemba 11, mwaka jana
akikabiliwa na kesi za uchochezi dhidi ya Rais Dk. John Magufuli na hadi wakati
huo bado anashikikiwa mahabusu katika gereza hilo.
Januari 4, mwaka huu Mahakama Kuu Kanda ya Arusha
inatarajia kutoa uamuzi wa rufaa namba 135 ya mawakili wa Serikali waliyokata
kupinga uamuzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha uliompa Lema dhamana, hata
hivyo uamuzi huo haukuweza kutekelezwa kwa sababu ya nia ya kukata rufaa
waliyoitoa mawakili hao wa Serikali.