CHADEMA YAWA MBOGO SASA,YAWASHUGHULIKIA WABAYA WA CHAMA SOMA HAPO KUJUA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani
Tabora, kimewasimamisha kazi kwa muda usiojulikana Mwenyekiti chama hicho
wilaya ya Igunga,Joseph Kashindye na Katibu wake, Idd Athuman.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani hapa
Katibu wa Chadema Mkoa wa Tabora, Ally Mwakilima alisema viongozi hao
wamesimamishwa uongozi tangu Novemba 30, mwaka huu baada ya kukiuka katiba ya
chama hicho.
Alisema kuwa uamuzi ya kuwasimamisha yametolewa na
baraza la uongozi la mkoa kupitia chama hicho baada ya viongozi hao wawili
kukiuka na kuvunja katiba ya chama ibara ya 10:3(4)(maadili ya wanachama).
Katibu huyo alisema tarehe Novemba 28 mwaka huu,
viongozi hao wawili walisimama mbele ya mahakama ya wilaya iliyopo mjini Tabora
kutoa ushahidi upande wa mtu aliyeshitaki chama huku wakiwa wanajua wazi kuwa
ni kinyume na katibu ya chama ibara ya 10:3 kifungu cha (4) maadili ya
wanachama.
Aidha katibu huyo alibainisha kuwa pamoja na
kuwasimamisha viongozi hao, pia baraza la chama hicho limemuagiza katibu wa
wilaya wa chama hicho, Idd Athuman kukabidhi mali zote za chama kwa katibu wa
jimbo la Igunga mbele ya mwenyekiti wake ikiwa ni pamoja na kujieleza ndani ya
siku 14.
Athumani na Kashindye wamekiri kupokea barua ya
kusimamishwa tangu Desemba 3, mwaka huu yenye kumbukumbu namba CDM/M/TBR/WG/01.
Hata hivyo, Athumani alisema yeye haoni kosa lolote
kwa kuwa aliitwa na mahakama kwenda kutoa ushahidi wa mwanachama aliyekwenda
mahakamani kutafuta haki ambayo hakupewa na chama.
“Kama kuitwa mahakamani kutoa ushahidi kuwa ni kosa
basi katibu wa mkoa hana kosa kunisimamisha uongozi lakini kama si kosa
kusimamishwa uongozi kumetoka wapi? alihoji katibu.
Sambamba na hayo katibu huyo alibainisha kuwa yeye
ataendelea kuwa mwanachama kwa kuwa chama chake bado anakipenda na hatasita
kutoa ushirikiano wakati wowote atakapohitajika.
Kwa upande wao baadhi ya wanachama wa chama hicho
ambao hawakutaka majina yao kuandikwa katika gazeti, wamesema viongozi wa mkoa
na wilaya wanapaswa kukaa meza moja kwa kuwa viongozi wao Athumani na Kashindye
hawaoni kosa walilofanya kwani wao waliitwa na mahakama.