SAKATA LA MBUNGE LEMA LACHUKUA SURA MPYA,AAMUA HAYA ,SOMA HAPO KUJUA
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema
ameamua kufunga ili kuwa karibu na Mungu wakati akiendelea kushikiliwa na
polisi mkoani Arusha.
Wakati Lema akiamua kufanya hivyo, taarifa
zilizopatikana mjini Arusha zinaeleza kuwa polisi walikwenda naye nyumbani
kwake kwa ajili ya upekuzi lakini hawakufanikiwa kupata chochote.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo
hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo na hata alipotafutwa kwa simu,
hakupokea.
Suala la Lema kuacha kula ili awe karibu zaidi na
Mungu lilielezwa na mwenyekiti wa Chadema wa mkoa, Amani Golugwa ambaye alisema
ameelezwa na mke wa mbunge huyo.
Lema, ambaye alikamatwa Jumatano iliyopita mkoani
Dodoma na kuletwa mjini hapa Alhamisi, bado hajafikishwa mahakamani. Imeelezwa
kuwa viongozi wa chama chake wameshindwa kumuona kutokana na kuzuiwa na
polisi.
Akizungumzia suala hilo jana, Golugwa alisema alipokea
ujumbe kutoka kwa mke wa mbunge huyo, Neema Lema kuwa mumewe ameamua kufunga na
kuomba kwa ajili ya Taifa kuhusu mambo yanayoendelea na kuwa ameona kipindi
hiki ambacho yupo rumande ni cha kuwa karibu zaidi na Mungu.
“Kama tunavyomjua Lema ni mtu anayempenda
sana Mungu, ameamua kujinyenyekeza mbele za Mungu. Anafunga na kuomba jioni mke
wake anampelekea chakula na amesema yupo katika hali nzuri,”
alisema Golugwa.
Golugwa alisema wamejitahidi kutaka kumuona Lema,
lakini wamegonga mwamba na wameshindwa kumwekea dhamana mbunge huyo.
Alisema alizungumza na ofisa upelelezi wa makosa ya
jinai mkoani hapa na Kamanda Mkumbo, wote walisisitiza kuwa Lema ataendelea
kuhojiwa hadi watakapojiridhisha.
“Ni jambo la kushangaza kama mtuhumiwa
anaweza kukaa rumande zaidi ya saa 48 kama sheria inavyotaka, nadhani hapa siyo
sheria tena, labda ni kwa mujibu wa maelekezo ambayo hatujui yametoka wapi na
kwa malengo yapi,” alisema Golugwa.
Alisema baada ya kuwasili kutoka Dodoma
alifanikiwa kuonana naye mara moja tu na baadaye hakuna mtu aliyeruhusiwa
kuonana naye; iwe viongozi wa Chadema au wakili wa chama hicho, John Mallya
ambaye ameshawasili kwa ajili ya mambo ya kisheria .
Juzi, Kamanda Mkumbo alisema Lema hataachiwa hadi
upelelezi ukamilike na mwanasheria wa Serikali atakapokuwa amemaliza kuandaa
mashtaka kwa kuwa amekuwa akirudia makosa yaleyale ya uchochezi.