BENKI YA TWIGA BANCORP KUANZA KUTOA HUDUMA ,NI ILE ILIYOANGUKA,SOMA HAPO KUJUA
Kwa mamlaka iliyopewa kisheria kupitia kifungu namba
58(2) (a) na (b) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, Benki
Kuu inapenda kuutarifu umma kwamba zoezi la tathmini ya hali ya kifedha ya
Twiga Bancorp Ltd (Twiga) limekamilika; kwa mantiki hiyo, Twiga itaanza kutoa
baadhi ya huduma za kibenki kwa umma kuanzia Jumanne tarehe 8 Novemba
2016.
Huduma hizo ni pamoja na ukusanyaji wa marejesho ya
mikopo ya wateja. Meneja Msimamizi wa benki hiyo atawajulisha wateja huduma
zitakazotolewa na taratibu za kuzingatia.
Benki Kuu ipo katika mchakato wa kupitia na
kuchambua njia mbadala za kutatua tatizo la mtaji linaloikabili Twiga Bancorp.
Njia inayopewa kipaumbele ni kutafuta mtaji kutoka kwa wawekezaji wapya,
mchakato utakaowahitaji kuchambua hali halisi ya taarifa za hesabu za Twiga
(due diligence).
Zoezi hili linatarajiwa kuchukua takribani
wiki tatu na litakapokamilika, Benki Kuu itaingia makubaliano na wawekezaji
wapya kuhakikisha wanaingiza mtaji unaohitajika haraka iwezekanavyo ili
shughuli za kawaida za kibenki ziweze kuendelea.
Benki ya Twiga itaendelea kuwa chini ya usimamizi wa
Benki Kuu hadi hapo utaratibu wa kuwamilikisha wawekezaji wapya
utakapokamilika.
Benki Kuu ya Tanzania ilitangaza kuiweka Twiga
Bancorp Ltd chini ya usimamizi wake kuanzia tarehe 28 Oktoba 2016 kutoka na
upungufu mkubwa wa mtaji unaoikabili.
Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuhakikishia umma
kuwa itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la
kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.
BENKI KUU YA TANZANIA
6 Novemba, 2016