RAIS MAGUFULI AMLILIA SAMWEL SITTA,SOMA HAPO KUJUA
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai kufuatia kifo cha Spika Mstaafu na Mbunge
Mstaafu wa Jimbo la Urambo lililopo Mkoani Tabora Mhe. Samwel Sitta.
Mhe. Samwel Sitta amefariki dunia usiku wa kuamkia
leo katika hospitali ya Technical University of Munich nchini Ujerumani
alikokuwa akipatiwa matibabu tangu mwezi uliopita.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli amesema amepokea
kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mhe. Samwel Sitta na
kwamba Taifa limempoteza mtu muhimu aliyetoa mchango mkubwa katika uongozi na
maendeleo.
“Nitamkumbuka Mzee Sitta kwa uchapakazi
wake, uzalendo wake na tabia yake ya kusimamia ukweli katika kipindi chote
alichokuwa kiongozi katika ngazi mbalimbali za siasa na Serikali.
“Kupitia kwako Mhe. Spika naomba kutoa
pole nyingi kwa Mke wa Marehemu Mhe. Magreth Sitta ambaye ni Mbunge wa Jimbo la
Urambo na familia nzima ya marehemu, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Wananchi wa Urambo Mkoani Tabora na watu wote walioguswa na msiba
huu”
amesema Rais Magufuli katika salamu hizo.
Dkt. Magufuli amesema anaungana na wafiwa wote
katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo na amewaombea moyo wa uvumilivu na
ustahimilivu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu aiweke roho ya
Marehemu mahali pema peponi, Ameni”
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
07 Novemba, 2016