PROFESA LIPUMBA NA MSAJILI WAKE WAGEUZIWA KIBAO,MAHAKAMA YAWABANA,SOMA HAPO KUJUA
Mahakama Kuu imewapa siku saba Msajili wa Vyama vya
Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba na wenzake kujibu madai ya chama hicho.
Msajili, Lipumba na wenzake walipewa muda huo jana
na Jaji Sekieti Kihiyo kutokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na Bodi ya
Wadhamini wa CUF mahakamani hapo.
Katika kesi hiyo namba 23 ya mwaka 2016, bodi ya
wadhamini CUF inaiomba mahakama itoe amri ya kubatilisha barua ya Msajili
inayomtambua Profesa Lipumba kuwa ndiye mwenyekiti wa chama hicho.
Pia, wanaiomba mahakama itoe amri ya kumzuia Msajili
kufanya kazi nje ya mipaka yake ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yake
na pia itoe amri ya kumzuia Msajili kuingilia masuala ya kiutawala ndani ya
chama hicho.
Mbali na Msajili na Profesa Lipumba, wadaiwa wengine
katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na wanachama wengine tisa
waliosimamishwa uanachama wa chama hicho, akiwamo Naibu Katibu Mkuu Bara ambaye
pia ni Mbunge wa Kaliua (Tabora), Magdalena Sakaya.
Kesi hiyo ilitajwa jana mahakamani hapo kwa mara ya
kwanza tangu ilipofunguliwa Oktoba 19, mwaka huu na mahakama ikataka wadaiwa
kuwasilisha majibu ya madai hayo ya CUF, Novemba 17, mwaka huu.
Pia, Mahakama ilielekeza upande wa Maalim Seif
kuwasilisha majibu ya hoja za wadaiwa Novemba 23 na ikapanga kesi hiyo itajwe
tena Novemba 24, kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine.
Wadai katika kesi hiyo wanawakilishwa na mawakili
Juma Nassoro na Halfani Daim wakati Msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
wanawakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu (PSA), Obadia Kameya na Lipumba na
wenzake wakiwakilishwa na Mashaka Ngole.
Katika hati ya Kiapo kinachounga mkono maombi hayo,
Maalim Seif anadai kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka ya kuingilia
utendaji wa ndani wa Vyama vya Siasa.
Anadai kuwa Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya
nchi haimpi mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa chombo cha rufaa wala
kurejea mambo ya utawala ndani ya chama cha siasa.
Badala yake anadai mamlaka hayo yako kwa vyombo vya
juu vya chama na Mahakama na kwamba jukumu la Msajili ni kusajili vyama na
kuweka kumbukumbu za vyama hivyo.
CUF kimekuwa na mgogoro wa kiuongozi baada ya
Profesa Lipumba kuandika barua ya kutengua uamuzi wake wa awali wa kujiuzulu
ambao Msajili alikubaliana naye na alikiandikia barua chama kuendelea kumtambua
mwenyekiti huyo. Hata hivyo, CUF ilimfukuza uanachama Lipumba.