SERIKALI YAENDELEA KUMNG'ANG'ANI MBUNGE LEMA,MKE WAKE ASEMA LEMA YUMO KWENYE MAPAMBANO YA KUDAI HAKI,SOMA HAPO KUJUA
Ujanja wa kisheria uliosababisha mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema kukaa mahakamani kwa saa 10, umemfanya kada huyo wa
Chadema kukosa tena dhamana.
Jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi ilishatupilia mbali hoja za Serikali za kupinga dhamana ya mbunge huyo, lakini mawakili walitumia silaha nyingine ya kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa kumpa dhamana Lema.
Jana, Mahakama ya Hakimu Mkazi ilishatupilia mbali hoja za Serikali za kupinga dhamana ya mbunge huyo, lakini mawakili walitumia silaha nyingine ya kukata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa kumpa dhamana Lema.
Mawakili wa Serikali walifanya hivyo muda mfupi baada
ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Arusha, Desderi Kamugisha kutupa hoja
za kuzuia dhamana ya Lema na hivyo kumzuia hakimu kuendelea na utaratibu wa
kumwachia mbunge huyo kusubiri uamuzi wa rufaa hiyo, hali iliyoibua vilio
mahakamani.
Kutokana na maamuzi hayo, hatma ya Lema kupata
dhamana inasubiri Mahakama Kuu kupanga jaji wa kusikiliza shauri hilo.
Lema, ambaye alifikishwa mahakamani saa 2:00
asubuhi, alirudishwa mahabusu akiwa kwenye basi la magereza lililokuwa na
ulinzi mkali saa 11:00 jioni.
Katika uamuzi wake uliotupilia hoja za awali za
Serikali kupinga dhamana, Hakimu Kamugisha alisoma maamuzi kwa saa 2:35 na
kutoa dhamana kwa Lema.
Hakimu Kamugisha alisema upande wa mashtaka
uliwasilisha hoja tatu za kupinga dhamana ya Lema katika kesi za uchochezi
namba 440 na 441/2016 na hati ya kiapo ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa
Arusha(RCO).
Alisema hoja ni kuwa mshtakiwa ametenda makosa hayo,
wakati akiwa nje kwa dhamana kwa kesi namba 351 na 352 za mwaka 2016, jambo
ambalo ni kinyume cha sheria.
Hakimu Kamugisha alisema hoja nyingine ni kutaka
Lema anyimwe dhamana kwa ajili ya kulinda usalama wake, hasa kwa kuwa kauli
zake za uchochezi dhidi ya Rais John Magufuli zimewaudhi wananchi.
Hoja ya tatu kujali maslahi ya Taifa. Hoja hizo
ziliandamana na hati hiyo ya kiapo cha RCO.
Hata hivyo, hakimu alisema mawakili wa utetezi
waliokuwa wanaongozwa na John Mallya walipinga hoja hizo, wakisema dhamana ni
haki ya mshitakiwa na kuwa nje kwa dhamana katika mashauri mengine ambayo
hayajamtia hatiani mtuhumiwa, hayawezi kuwa sababu ya kumnyima dhamana.
Alisema mawakili hao, pia walipinga hoja za
kutokutolewa dhamana kutokana na usalama wake na maslahi ya Jamhuri na pia
wakakosoa hati ya kiapo kuwa ina mapungufu, hasa ya kutokuwa na uthibitisho wa
mambo yaliyoelezwa.
Hakimu Kamugisha alisema msingi wa haki ya dhamana
ni wa Katiba ibara ya 15(1) na (2) ambayo inaelezea uhuru wa mtu.
Alisema pia ibara ya 17 ya Katiba inatoa haki ya mtu
kutembea popote na kuongeza ibara ya 16(6) B inaeleza mahakama inamchukulia
mtuhumiwa yeyote kuwa hajafanya kosa hadi anakapotiwa hatiani.
Alisema washitakiwa hupelekwa mahabusu ili iwe
lazima mtuhumiwa kufika mahakamani.
Hakimu Kamugisha alisema, siku zote dhamana
haitolewi ikiwa tu kuna mazingira ya kisheria ambayo yameelezwa na kuwekewa
masharti na utaratibu wake.
Alitolea mfano kesi ya Mkurugenzi wa Mashitaka(DPP)
dhidi ya Daudi Beda ambapo ilielezwa haki za mshtakiwa na sababu ambazo
zinaweza kuzuia dhamana.
Alisema katika kesi hiyo, mahakama iliamua kuwa ili
kunyimwa dhamana lazima kuwepo mazingira yaliyoanishwa kisheria na utaratibu
ulioanishwa kisheria.
“Nimeshindwa kupata kifungu chochote cha
sheria ambacho kinazuia kutoa dhamana kwa mtuhumiwa aliye nje kwa dhamana
ambaye ametenda makosa mengine ambayo hayahusiani na masharti ya dhamana ya
awali,” alisema.
Alisema hata maelezo kuwa watu waliohudhuria mkutano
hawakuridhishwa na kauli za Lema na kwenda kulalamika kwa RCO, hayana
panapoonyesha usalama wa mtuhumiwa upo mashakani.
Alisema ili hoja ya dhamana izuiwe kwa maslahi ya
Jamhuri, inakuwa na hati ya maombi hayo iliyotolewa na Mkurugenzi wa
Mashitaka(DPP) na si RCO hivyo haoni msingi wa kutotoa dhamana hiyo “Hivyo kwa
uchambuzi huu wa kisheria natoa dhamana kwa mshitakiwa,” alisema.
Hata hivyo, wakati anajiandaa kuandika masharti ya
dhamana, ndipo wakili mwandamizi wa Serikali, Paul Kadoshi aliwasilisha notisi
za kupinga uamuzi wa dhamana hiyo.
Alisema anawasilisha notisi hiyo chini ya kifungu
cha 379 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 ya mwaka 2002.
Alisema nia ya kuwasilisha notisi hiyo inatokana na
mabadiliko ya Sheria za Makosa ya Jinai namba 27 ya mwaka 2008.
Alisema kifungu cha 31 aya G katika sheria hiyo
kifungu 379(1 ) (a) kwa kuongeza maneno kuwa notisi ya kukata rufaa inaweza
kujulikana kama ni rufaa.
Alisema mabadiliko ya sheria hiyo yalimpa hadhi DPP
anapoeleza notisi ya rufani kuwa tayari ni rufani kamili na hivyo notisi hiyo
ikitolewa mwenendo wa kesi nzima unapaswa kusimama.
Kadoshi alisema maamuzi hayo, yamefikiwa katika kesi
ya Jamhuri dhidi ya Harry Kitillya na wenzake wawili, pale DPP alipowasilisha
notisi na rufani na kesi kusimama.
Hata hivyo, licha ya mawakili wa utetezi, Sheki
Mfinanga na Richard Shediel kupinga hoja hiyo, Haklimu Kamugisha, ambaye
aliomba dakika 10 kutafakari suala hilo, alikubaliana na hoja za upande wa
Serikali za kumkatalia Lema dhamana.
Kutokana na maamuzi hayo Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema, Salum Mwalimu amesema chama hicho kimewataka wanasheria wake, Tundu
Lissu na Peter Kibatala kwenda Arusha kuongeza nguvu katika kudai haki ya Lema
kuwa huru.
Mke wa Lema, Neema Lema aliwataka wakazi wa Arusha
kuwa watulivu, akisema mbunge huyo anapigania uhuru wa wananchi.