MBUNGE LEMA NA MKEWA MATATANI TENA,SOMA HAPO KUJUA
Neema Lema (33), mke wa Mbunge wa Arusha
Mjini, Godbless Lema (Chadema), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Arusha.
Alifikishwa mahakamani hapo jana na
kuunganishwa katika kesi ya tuhuma za kusambaza ujumbe unaomkashifu Mkuu wa
Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.
Katika kesi hiyo ya jinai namba 351 ya mwaka huu,
mshitakiwa mwingine ni Lema ambaye alifikishwa mahakamani hapo Agosti 20 mwaka
huu.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Agustine Rwizile, Wakili wa Serikali, Blandina Msawa, aliiomba
mahakama kufanya marekebisho kwenye hati ya mashtaka kwa kumuongeza
Neema.
Akisoma mashtaka yanayomkabili Neema, wakili huyo
alidai Agosti 20 mwaka huu, jijini Arusha, mshtakiwa alituma ujumbe
kwa simu ya mkononi uliosema, ‘karibu tutakudhibiti kama Uarabuni
wanavyodhibiti mashoga’.
Neema anayetetewa na Wakili Sheck Mfinanga, alikana
kutenda kosa hilo na kupewa dhamana hadi Novemba 15, mwaka huu, kesi hiyo
itakapotajwa tena.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Arusha,
lilimkamata na kumhoji Lema kwa tuhuma za kutoa lugha za uchochezi dhidi ya
Rais Dk. John Magufuli.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa
Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema Lema alitoa lugha hiyo wiki
iliyopita katika mikutano halali aliyoifanya jimboni kwake.
“Tumemkamata Lema kwa kutoa lugha ya
uchochezi ambayo ni kinyume cha sheria.
“Baadhi ya maneno aliyotoa yenye
uchochezi ni pamoja na kusema Rais Magufuli
akiendelea kugandamiza demokrasia, taifa litaingia katika umwagaji wa damu,
nchi hii inaandaliwa kwenda katika utawala wa udikteta pamoja na kuwataka
wananchi wawe tayari kwa lolote na waache uoga kwa vile uoga ni
dhambi mbaya kuliko dhambi zote duniani.
“Baada ya kumhoji kuhusu maneno hayo,
tulimwachia kwa dhamana na sasa jalada lale liko kwa Mwanasheria wa Serikali
kwa ajili ya kuandaa hati ya mashitaka afikishwe mahakamani,” alisema
Kamanda Mkumbo.