SUMAYE ASEMA KUWA CHAMA CHA UPINZANI KUNATAKA MOYO,SOMA HAPO KUJUA
WAZIRI Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, amekiri kuwapo
na ugumu wa kufanya siasa nje ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwataka
wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kujitoa na kufanya
kazi kwa moyo.
Sumaye ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema
alitoa kauli hiyo Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani jana wakati wa shughuli ya
kuchangia ujenzi wa Ofisi ya Chadema iliyopo wilayani humo.
Alisema wanachama wa chama hicho kuanzia ngazi ya
chini wanapaswa kujitoa katika shughuli za ujenzi wa chama ili kuweza kufikia
lengo la kushika dola ifikapo mwaka 2020
.
“Ninaamini wote tuliopo tutajitoa kwa moyo mmoja,
najua ni kazi ngumu kuwa na chama tofauti na chama tawala lakini tunapaswa
kupambana kufikia malengo,” alisema.
Sumaye ambaye kabla ya kampeni za Uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana hazijaanza alijitoa CCM na kuhamia Chadema
kwenda kumwongezea nguvu aliyekuwa mgombea urais wa Chadema chini ya mwavuli wa
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
alisema kwa sasa hata CCM inajua kuwa Chadema itashika dola hivyo vijana
wakijenge kuanzia ngazi ya matawi.
“Lazima tujitolee, dola haipatikani kiurahisi,
tunapaswa tuwaeleze wananchi tutawafanyia nini, hatuwezi kufanya kazi za chama
kwenye nyumba ya mtu au ofisi za vichochoroni kuanzia mwaka 1992,” alisema
Sumaye.
Naye Katibu Mkuu Taifa wa Chadema, Vicent Mashinji,
alisema kwa sasa ni wakati wa kudai Katiba Pendekezwa iliyokuwa ikisimamiwa na
Jaji mstaafu Joseph Warioba, ili kupunguza madaraka ya rais.
“Tunahitaji Katiba ya wananchi, tunapaswa kufanya
hii kampeni kwa ngazi ya msingi, tunahitaji rais hatuitaji Mungu, rais asiseme
mimi sichezewi kwa sababu yeye si Mungu, ambaye hachezewi ni Mungu tu binadamu
wote kuna aina ya kuchezeana,” alisema Mashinji.
Pia alisema Katiba mpya itasaidia kupata tume huru
ya uchaguzi huku akirejea uchaguzi wa marudio uliofanyika Zanzibar Machi 21,
mwaka huu na kudai kuwa Serikali imekuwa ikifanya mambo kwa kukurupuka bila
kufuata sheria za nchi.
“Siamini kama miaka yote tutavumilia, uvumilivu una
kikomo, tunalalamika lakini inawezekana safari ijayo wakalalamika wao, kila
siku mnasema hatushindi tutashinda tu,” alisema Mashinji.
Alisema kwa mwenendo wa Serikali iliyopo bila Katiba
mpya nchi inaweza ikaingia katika machafuko bila sababu za msingi.
Mashinji alisema Taifa linabomoka kuanzia juu kwenda
chini na itakuwa ngumu kuliokoa.
Alisema katika uongozi demokrasia ni suala la msingi
na si kuongoza nchi kwa matamko na amri.
Katika hafla hiyo, jumla ya Sh milioni 9.9
zilipatikana ikiwamo ahadi na kati ya hizo Sh milioni tatu zilitolewa na Dk.
Mashinji