MBUNGE WA KENYA AMPA USHAURI RAIS MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA
Mbunge wa Budalang’i nchini Kenya, Ababu Namwamba
amesema Rais John Magufuli anavuma kwa umashuhuri nchini humo akitajwa kwa
namna anavyopambana na ufisadi na kubana matumizi ya Serikali, lakini akasema
sifa hizo zitapendeza iwapo huduma muhimu kwa wananchi zitaboreshwa na
kuthibitika kwenye tafiti zitakazofanywa.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati
alipohudhuria mkutano wa demokrasia ulioandaliwa na ACT – Wazalendo jana,
Namwamba ambaye pia ni kiongozi wa chama cha Labour of Kenya (LPK), alisema
Rais Magufuli ana mtandao Kenya unaomshabikia kwa uongozi wake, ikiwamo
harakati zake za kupambana na ufisadi
“Lakini swali kuu katika fikra za
Wakenya wengi ni sasa je, mambo yote tunayoona kwenye vyombo vya habari ni
porojo tu ama ile inaitwa propaganda au ni masuala kweli yanayobadili maisha ya
Watanzania wengi? Hivyo ingawa sifa za Magufuli zinaenea huku na kule,
tungependa kuona mabadiliko halisi hapa Tanzania,” alisema.
“Tungependa kuona kwa mfano takwimu za
ufisadi zimepungua. Takwimu za kuonyesha hali ya maisha ya Mtanzania wa kawaida
imebadilika huduma kama vile maji, elimu na afya kwamba kweli zimebadilika hilo
ndilo la muhimu zaidi, kinyume cha hapo hatutapata sababu ya kuamini au kuona
kwamba mabadiliko hayo ni halisi.”
Namwamba, ambaye Julai 7 mwaka huu alijiuzulu
ukatibu mkuu wa chama cha ODM kinachoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Raila
Odinga baada ya kutoelewana, alisema siasa za nchi hizo mbili zinakaribiana kwa
kuwa mashindano ya wanasiasa yaliyopo nchini ni kama yalivyo Kenya.
“Kila mara mnapokuwa na uchaguzi
hapa sisi hutazama kwa makini sana kwa sababu kuna mengi ya kujifunza.
"
Hata hivyo, Namwamba alionya kuwa suala la
ukabila nchini ni la kutiliwa maanani kwa kuwa kufanya siasa kwa misingi hiyo
kumesababisha maafa makubwa ikiwamo mgawanyiko kwa wananchi.
Alisema siasa nzuri zinazopaswa kuendelezwa
nchini ni zile za kuwaleta wananchi pamoja na kama ni mashindano, yawe ya sera,
dhana, huduma bora kuliko kumtazama kiongozi wa chama au mgombea kwa kabila
lake.
Alisema amekuja nchini kushirikiana na Kiongozi wa
ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe kupanda mbegu ya ushirikiano na kwamba atashiriki
kuhamasisha vijana kutambua viongozi walioweka historia wakiwamo Mwalimu Julius
Nyerere na Nelson Mandela.
Zitto akizungumza katika mkutano huo alieleza
kuwa chama chake kinaunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Magufuli katika
kurejesha nidhamu ya kazi kwa watumishi wa umma na kupambana na ufisadi.
“Lakini tungependa kuona hatua
zinachukuliwa zaidi ikiwa ni pamoja na kuwafikisha kwenye vyombo vinavyohusika
watumishi 154 wachukuliwe hatua zinazostahili.Pia suala la Escrow nalo
linapaswa kuchukuliwa hatua na mengine mengi.”
Mshauri wa ACT, Profesa Kitila Mkumbo aliwasilisha
mada ya; “Sisi ni kina nani?” akilenga kuwaelimisha wanachama wake kujihusisha
na maisha ya watu, kwa kuwa kushughulikia changamoto na matatizo ni mchakato
unaoendelea iwe ndani au nje ya Serikali.
“Chama chetu siyo cha kuvizia makosa ya
Serikali ndipo tufanye siasa, tunajipanga kushindanisha ubora wa sera, kina
itikadi yake kamili, ni jukumu letu kukosoa Serikali lakini jambo la muhimu ni
kuonyesha tuna vitu gani bora kwa wananchi.”
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba
ambaye alitoa mada iliyohusu masuala ya Katiba alisema mchakato wa Katiba hauna
budi kurudishwa nyuma kwa hatua moja hadi kwenye rasimu.
“Kuna mambo mengi yamejitokeza ambayo
yamewachanganya wananchi, hivi sasa wengi wanatofautiana hawajui uliishia
kwenye hatua gani. Pia, hali iliyojitokeza kule Zanzibar ambapo wakati
unajadiliwa awali kulikuwa na Serikali ya umoja ambayo sasa haipo. Kuna mambo
mengi ambayo tumekuwa tunarudi nyuma hatua tano kisha kwenda mbele hatua
mbili.”