SERIKALI YAANGUKA TENA MAHAKAMA,KESI ZA MITANDAO ZAZIDI ITESA,SOMA HAPO KUJUA
Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo cha
Maendeleo ya Jamii (CDTI) cha mkoani Arusha, Allan Mbando, ameibwaga Serikali
katika kesi ya kudaiwa kusambaza ujumbe kupitia Mtandao wa Facebook akimtaka
Mwamunyange apindue nchi.
Katika mtandao huo wa kijamii, Mbando, anadaiwa
kutuma ujumbe uliosomeka kwamba: “Mwamunyange pindua nchi haiwezekani
wote wawe nje, halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile kiti.”
Kutokana na madai hayo, Jeshi la Polisi mkoani
Arusha lilimfungulia mashtaka Mbando ya kudaiwa kusambaza ujumbe huo
uliokusudia kueneza na kufanya uchochezi.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo mjini hapa juzi, Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Augustine
Rwizile, alisema mahakama hiyo imepitia kwa kina hoja na ushahidi wa pande zote
mbili katika kesi hiyo.
Hakimu Rwizile alisema baada ya kupitia ushahidi
katika kesi hiyo, mahakama imejiridhisha kuwa upande wa Jamhuri katika kesi
hiyo haukuweza kuwasilisha ushahidi unaoweza kumtia hatiani mshtakiwa.
Alisema mbali na ushahidi huo kutojitosheleza, pia
hapakuwapo na jambo lolote lenye nia ovu ya kusababisha au kufanya uchochezi
katika ujumbe uliosambazwa na mshtakiwa.
“Sasa mahakama hii inamwachia huru
mshtakiwa baada ya upande wa Jamhuri kushindwa kuthibitisha mashtaka yake
pasipo kuacha shaka yoyote.
“Lakini pia kama kutakuwa na upande
ambao haujaridhika katika hukumu hii unaweza kukata rufaa,” alisema
Rwizile.
Akisoma hukumu hiyo, alisema ujumbe uliosambazwa
haukuwa na umuhimu wowote kwa kuwa haukumwelezea Mwamunyange ni nani katika
nchi anayotakiwa kuipindua huku pia ujumbe huo ukiwa haukutaja nchi iliyolengwa
kupinduliwa.
“Ujumbe ulioandikwa katika Facebook
haumtambulishi Mwamunyange ni nani. Lakini ujumbe hauonyeshi jambo la msingi lenye
uhusiano wa kisiasa katika Taifa linalodaiwa,” alisema
Rwizile.
Kutokana na sababu hizo ikiwamo ushahidi
uliowasilishwa mahakamani hapo kushindwa kuthibitisha ujumbe uliosambazwa na
mshtakiwa, mahakama ililazimika kumwachia mshtakiwa.
Mshtakiwa huyo katika kesi hiyo alikuwa akitetewa na
Wakili Moses Mahuna.
Mbando anaongeza idadi ya watu walioshtakiwa
mahakamani kutokana na makosa ya mtandaoni baada ya Aprili, mwaka huu mkazi
mwingine wa Arusha, Isack Habakuki (40), kufikishwa mahakamani na kusomewa
mashtaka ya kusambaza lugha ya matusi na dhihaka kwa Rais Dk. John
Magufuli.
Baada ya kesi hiyo kuendelea kusomwa mahakamani
hapo, Isack alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh
milioni saba na yeye alikubali kuzilipa kwa awamu.
Mtu mwingine aliyeshtakiwa Aprili, mwaka huu kwa
makosa ya mtandaoni ni kondakta wa daladala, Hamimu Seif (42), aliyepandishwa
kizimbani kwa kosa analodaiwa kulifanya Machi 10, mwaka huu alipotishia kumuua
Rais Magufuli kwa maneno akiwa katika Baa ya Soweto iliyopo Makumbusho, Wilaya
ya Kinondoni jijini Dar es Salaam