PROFESA LIPUMBA AZIDI GONGA MWAMBA,WANACHAMA WA CUF TANGA WAMKATAA MAZIMA,SOMA HAPO KUJUA
CHAMA cha Wananchi (CUF) wilayani hapa kimetoa tamko
la kutomtambua Mwenyekiti wa Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, na kwamba
hakitampokea katika ziara yake.
Lipumba anatarajia kuanza ziara mkoani Tanga
kesho huku uongozi wa chama hicho ukisisitiza kutambua uamuzi wa
Mkutano Mkuu uliomwondoa madarakani na wa Baraza Kuu kumvua uanachama.
Mwenyekiti wa CUF wa Wilaya ya Tanga, Rashid Jumbe
alitoa tamko hilo jana akieleza kuwa hawatakuwa tayari kukaidi Katiba ya Chama
chao na kwamba hawatampokea na hakuna maandalizi yatakayofanyika kumpokea.
"Tumeambiwa Lipumba ana dhamira ya
kufanya ziara mkoani hapa. Sisi kwa uamuzi wa Baraza hatumtambui, wala
hatujaandaa maandalizi ya kumpokea.
“Wilaya za Korogwe na Muheza ndizo
zimesema atazitembelea, lakini sisi hatuko pamoja nao na watakaompokea
wataingia kwenye mgogoro mwingine kwa sababu hatambuliki," alisema
Jumbe.
Mwenyekiti huyo pia alizungumzia mgogoro baina yao
na CCM kutokana na sakata la umeya ambapo alisema hatima ya mgogoro huo
itajulikana baada ya mkutano mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29.
Alisema kutokana na sakata hilo walitoa malalamiko
kwa viongozi mbalimbali lakini hakuna hatua zozote zinazoendelea, hivyo Kamati
ya Utendaji iliwataka madiwani wa chama hicho kutohudhuria kikao chochote cha
Halmashauri hadi itakapotoa uamuzi.
"Tumetoa malalamiko yetu kwa
viongozi wa CCMna lengo letu ilikuwa tuonane na Rais lakini tulimpata
Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa aliyetwambia kuwa atalifanyia kazi, lakini sasa
tumeamua kupeleka malalamiko yetu kwa wenye chama na wao ndio watakaotoa uamuzi
juu ya mgogoro huo.
“Hivyo tumeitisha mkutano ambao utakuwa
na wajumbe 440 ambapo tuna imani kuwa tatizo letu litakwisha Oktoba 29,” alisema
Jumbe.