MAWAZIRI WAKUU WASTAAFU KUWAFUNDA WABUNGE WA UKAWA KIMAPAMBANO,SOMA HAPO KUJUA
Mawaziri Wakuu wa zamani ambao ni wajumbe wa
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa
na Frederick Sumaye wameweka kambi mjini Dodoma ili kuteta na wabunge wa Ukawa.
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo
ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kuwa wanasiasa hao wako mjini humo kwa
ajili ya kufanya vikao na wabunge wa Ukawa ili kuweka mkakati na msimamo dhidi
ya hoja mbalimbali zinazotarajiwa kuibuliwa katika vikao vya Bunge vinavyoanza
kesho.
Moja kati ya hoja zinazotarajiwa kuwekewa msimamo ni
pamoja na kuupinga muswada wa huduma za habari unaotarajiwa kujadiliwa na
kupitishwa kuwa sheria.
“Tutakuwa na kikao cha kuweka msimamo
wetu dhidi ya muswada hatari wa huduma za habari,” Mrema
anakaririwa. “Vikao vimeshaanza na vitaendelea kesho (leo),”aliongeza.
Kwa mujibu wa Mrema, mbali na Lowassa, Sumaye na
mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, vigogo wengine wa Ukawa waliohudhuria
vikao hivyo ni pamoja na Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na
Arcado Ntagazwa.