HABARI NJEMA,TANZANIA YAANZA KUTENGEZA MAGARI,SOMA HAPO KUJUA
KAMPUNI ya Simba Motors imesema ina mpango wa
kujenga kiwanda cha kuunganisha magari aina ya pick-up ambacho kitaanza
kuzalisha magari kabla ya Desemba 30, mwaka huu.
Ahadi hiyo imetolewa jana mchana (Jumatatu, Oktoba
10, 2016) na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Jitesh Ladwa mbele ya
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwake
Magogoni, jijini Dar es Salaam.
“Tumeamua kuunda magari aina ya pick-up
kwa sababu ya mahitaji makubwa yaliyopo nchini. Takwimu zinaonyesha kuwa, kwa
mwaka Tanzania inanunua magari ya aina hii zaidi ya 4,000. Katika nchi za SADC
mahitaji ni pick-up 35,000 kwa mwaka. Tutaanza na mtaji wa dola za Marekani
milioni 200 na tumeomba ekari 200 katika eneo la EPZ,”amesema.
“Eneo la kiwanda cha kuunganisha magari
peke yake linahitaji ekari 50, kwa hiyo tukiweka na yadi za kupaki magari, eneo
la viwanda vingine, eneo la kushusha na kupakia makontena yatakayokuwa
yakisafirishwa kwenda nchi jirani, ni lazima tutahitaji eneo kubwa zaidi,” amesisitiza.
Amesema mradi huo wa majaribio, utaanza kwa
kutengeneza magari 20 kila mwezi na kwamba kazi ya utengenezaji magari
itaongezeka na kufikia 1,000 na baadaye 5,000 kwa mwaka. “Tunataraji gari la
kwanza litazinduliwa kabla ya Krismasi, mwaka huu,” amesema.
Bw. Ladwa amesema uundaji wa magari hayo aina ya
Foton-Tunland utafanyika kwa ubia baina ya kampuni yao, SUMA-JKT na kampuni
Foton International ya China kwa kutumia teknolojia ya Kichina na kwamba magari
hayo yanayotumia 4-Wheel Drive, yana uwezo wa kupita kwenye barabara za aina
zote.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa
Uendeshaji wa Kampuni hiyo, Bw. Aatish Ladwa, amesema mradi utakapoanza, mbali
ya kutoa ajira kwa Watanzania, utawezesha pia kujengwa kwa viwanda vingine
vitakavyotengeneza matairi ya magari, vioo, taa, bumpers, viti na filters.
“Tunataraji kujenga uwezo wa wahandisi
wazawa, uhamishaji wa ujuzi kwa mafundi wa Kitanzania (technology transfer),
kupunguza bei kwa mlaji wa mwisho, kupunguza gharama za uzalishaji, kutekeleza
amza ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa ni nchi ya viwanda, kuongeza ajira
kwa wanajeshi, na kuwezesha upatikanaji wa vipuri vya magari kwa urahisi na
kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.”
“Kiwanda kitaajiri wafanyakazi 1,500 kwa
kuanzia ambao watakuwemo mafundi na watoa huduma mbalimbali, lakini katika
kipindi cha miaka mitatu hadi mitano, tunataraji kuongeza wafanyakazi wengine
5,000 wakati uzalishaji ukiwa umepamba moto,” amesema.
Kwa upande wake, akizungumza mara baada ya kulikagua
gari la mfano aina ya Foton-Tunland, Waziri Mkuu amesema anawakaribisha kwenye
uwekezaji huo hasa ikizingatiwa kuwa magari hayo yana uwezo wa kupita kwenye
maeneo ya vijijini ambako barabara zake siyo nzuri.
“Ofisi za Serikali zinayahitaji zaidi
haya magari, hospitali zetu za wilayani nazo pia zinayahitaji haya magari ili
yaweze kutoa huduma za chanjo kwa watoto, huduma za UKIMWI, kampeni za
kupambana na malaria, na huduma kwa mama wajawazito huko vijijini,” amesema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,