SAKATA LA MELI ZA KOREA KUSAJILIWA NCHI,LAZIDI CHUKUA SURA MPYA,ZMA WAIBUKA,SOMA HAPO KUJUA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar
Mustafa Aboud Jumbe akitowa ufafanuzi wa masuala yaliyoulizwa na Waandishi wa Habari
katika Mkutano huo. (Picha na
Miza Othman Habari Maelezo Zanzibar).
Na Ramadhan Ali/Maelezo Zanzibar
11.10.2016
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar
(ZMA) imekanusha tuhuma zinazotolewa kuwa imesajili meli za Korea Kaskazini
kinyume na Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mwezi
Machi mwaka huu za kuzikatalia usajili Kampuni za meli za nchi hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari,
Mkurgenzi Mkuu wa ZMA Abdalla Hussein Kombo amesema tuhuma hizo zilizotolewa na
Mkurugenzi wa Habari na Uchambuzi wa Taasisi ya NK News kupitia Jarida la NK
Pro la Mjini Seoul, Korea Kusini sio za kweli.
Amesema ZMA baada ya kupata taarifa ya
Azimio hilo iliunda Kamati ya wataalamu kulifanyia uchambuzi na kutoa
mapendekezo kwa Mamlaka juu ya hatua za kuchukuliwa."Azimio hilo limetaja
majina ya meli 31 za Korea Kaskazini ambazo nchi zote wanachama wa Umoja wa
Mataifa, ikiwemo Tanzania, inazitaka kuzifutia usajili au kutozisajili,"
alisema Mkurugenzi Mkuu ZMA.
Aliongeza kuwa ZMA ilifanya uhakiki wa
meli zote zilizosajiliwa na Mamlaka hiyo na orodha ya meli zilizoainishwa
kupitia Azimio hilo na kubaini kuwa meli moja yenye jina la First Cleam ilikuwa
imesajiliwa kabla ya vikwazo vya usajili wa meli za Korea Kaskazini lakini
ikaamua kuifutia usajili.
Amesema kuanzia wakati huo, Mamlaka
haijawahi kusajili meli yeyote ambayo ilikuwemo katika orodha iliyotolewa na
Umoja wa Mataifa na imekuwa ikichukua tahadhari kubwa katika usajili wa meli.
Mkurugenzi Mkuu wa ZMA alisisitiza kuwa
ili kuhakikisha hawatoi usajili kwa meli zenye uhusiano na Korea Kaskazini
imekuwa ikishirikiana kwa karibu na Taasisi za Kimataifa ikiwemo IMO.
Hata hivyo amekiri kuwa Kampuni ya
Filtex ambayo ilikuwa wakala wa ZMA nchini Dubai na kuvunja naye mkataba bado
inaendelea kusajili meli kwa jina la Zanzibar kinyume na sheria.
Amesema tayari wameshawasiliana na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuifuatilia Kampuni hiyo na kuifungulia
mashtaka kwenye mahakama za Kimataifa.Amesema katika kukabiliana na uharamia
unaofanywa na Kampuni ya Filtex, miezi michache ijayo, ZMA itafungua Ofisi yake
nchi Dubai kwa ajili ya usajili wake wa meli wa Kimataifa.
Kufuatia majaribio ya Korea Kaskazini
kutengeneza silaha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika kikao chake
cha 7638 kilichofanyika tarehe 2 Machi, 2016 ilipitisha Azimio la kuiongezea
vikwazo Korea Kaskazini ikiwemo kuzinyima usajili meli zote za nchi hiyo ama
zenye uhusiano nazo.