FIGISU ZA UMEYA ZAANZA TENA KINONDONI,CHADEMA NA MKURUGENZI VITANI,SOMA HAPO KUJUA

Wakati mchakato wa uchaguzi wa meya na naibu wake
ukiendelea, suala la idadi ya madiwani wa viti maalumu wa Chadema katika
Manispaa ya Kinondoni limeibua mvutano mpya kati ya chama hicho na ofisi ya
mkurugenzi mtendaji.
Mvutano huo umejitokeza baada ya Mkurugenzi wa
Kinondoni, Aron Kagurumjuli kutoa barua inayoeleza kuwa kutakuwa na madiwani
viti maalumu wanawake wasiopungua theluthi moja ya madiwani wa kuchaguliwa wa
Chadema.
Kwa mantiki hiyo, Chadema ambayo ina madiwani wa
kuchaguliwa saba itakuwa na madiwani watatu wa viti maalumu. Kwa hiyo majina
yasiyopungua matatu ndiyo yatakayowasilishwa kuunda baraza jipya la madiwani.
Hata hivyo, Katibu wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam,
Henry Kilewo alipinga maelezo hayo ya mkurugenzi akisema: “Tayari
nimeshamwandikia barua mkurugenzi kumweleza. Tungekuwa tunatoka katika uchaguzi
mkuu ningekubaliana na hoja ya Kagurumjuli, lakini kwa hali ilivyo sasa siwezi
kukubaliana naye kwa sababu baraza likiitishwa madiwani hawatakula kiapo kama
awali.”
Kuhusu madai hayo Kagurumjuli alisema: “Nasimamia
sheria, sifuati matakwa ya mtu. Nadhani wao wanapingana na sheria. Sielewi
presha inatoka wapi. Wa kushinda atashinda na wa kukosa atakosa kulingana na
idadi ya wajumbe wake na hakuna atakayeonewa.”
Alisisitiza kuwa kulingana na sheria hiyo na idadi
ya madiwani wa kuchaguliwa wa Chadema, chama hicho hakiruhusiwi kuongeza diwani
mwingine. Kagurumjuli hakuwa tayari kutaja idadi ya wajumbe watakaounda baraza
la madiwani na kusema kwamba anasubiri majina ya madiwani kutoka CUF, Chadema
na CCM.
Lakini Kilewo alisema msimamo wa Chadema uko
palepale wa kuhakikisha madiwani wanne wanabaki Kinondoni na kwamba hakuna
mwenye mamlaka ya kuengua mjumbe isipokuwa kifo na mahakama.
“Ubungo hakuna tatizo. Ingawa maelezo
yanafanana ya wajumbe watatu kutakiwa kulingana na idadi ya madiwani wa
kuchaguliwa. Ishu ipo Kinondoni kwa sababu madiwani wetu wa viti maalumu wengi
walikubaliwa,” alisema Kilewo.
Kuhusu umeya baada ya manispaa hizo kugawanywa,
Kilewo alisema jina la Mustafa Muro, Diwani wa Kinondoni, ndilo
lililopendekezwa na kupelekwa kwa ajili ya kugombea umeya wa Kinondoni huku
Boniface Jacob akiteuliwa kugombea Ubungo.
Wakati Kilewo akisema hayo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya
ya Kinondoni, Salum Madenge alisema mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi ya umeya
na naibu meya katika manispaa hizo ulitarajiwa kukamilika jana jioni.
“Mchakato huu ulianza muda mrefu lakini
leo (jana), jioni ndiyo kilele chake. Wagombea watakaopatikana ni mahiri na CCM
ipo fiti tunasubiri mechi uwanjani,” alisema Madenge.
Kwa nyakati tofauti, Manispaa za Kinondoni na Temeke
zilifanya mgawanyo wa madiwani baada ya Serikali kuzigawanya na kuunda
halmashauri za Ubungo na Kigamboni.