SINEMA YA SCORPION YAFIKIA PATAMU,SOMA HAPO KUJUA

Mkazi wa Machimbo Yombo jijini Dar es Salaam,
Salum Njwele (34) maarufu kama Scorpion, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya
ya Ilala kujibu mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kumtoboa macho
yote mawili Said Mrisho.
Scorpion alifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya
Hakimu Mkazi, Adelf Sachore na kusomewa mashitaka na Wakili wa Serikali, Munde
Kalombola.
Akisoma mashitaka hayo, Kalombola alidai kuwa
mshitakiwa alitenda kosa hilo Septemba 6, mwaka huu eneo la Buguruni Sheli
wilaya ya Ilala.
Munde alidai, Njwele aliiba mkufu rangi ya fedha
wenye uzito wa gramu 34 ikiwa na thamani ya Sh 60,000, bangili na fedha taslimu
Sh 331,000 vyote kwa pamoja vikiwa na thamani ya Sh 476,000 mali ya Mrisho.
Kalombola alidai kuwa mshitakiwa kabla na baada ya
wizi huo, alimchoma kisu machoni, tumboni na mabegani mlalamikaji ili ajipatie
mali hizo.
Hata hivyo, upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na
upande wa mashitaka uliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutaja.
Hakimu Sachore aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 19,
mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena. Mshitakiwa alirudishwa rumande kutokana
na mashitaka yanayomkabili kutokuwa na dhamana.