CHADEMA YASHTUKIA FIGISU ZA UMEYA KINONDONI,SOMA HAPO KUJUA
CASIMIR Mabina, Katibu wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Kanda ya Pwani amesema wamejipanga kudhibiti hila za Chama
Cha Mapinduzi (CCM) kinachotaka kutwaa umeya wa Manispaa ya Kinondoni jijini
Dar es Salaam, kinyume na utaratibu, anaandika Pendo Omary.
Uchaguzi
wa Meya wa Manispaa ya Kinondoni utafanyika tena baada ya kugawanywa kwa
manispaa hiyo na kupatikana nyingine ya Ubungo, kwa lengo la kuongeza ufanisi
ikiwemo kusogeza karibu zaidi huduma kwa wananchi.
Akizungumza na mtandao huu siku ya leo, Mabina
amesema CCM inafanya hila za kupunguza madiwani wawili, mmoja kutoka Chadema na
mwingine Chama cha Wananchi- CUF katika Manispaa ya Kinondoni huku
wakikiongezea chama tawala diwani mmoja ili kutengeneza mazingira ya ushindi
usio halali.
“Chadema tuna madiwani 13, CUF 7 na CCM 16 kwahiyo
kwa ujumla vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) tuna madiwani 20 dhidi
ya 16 wa chama tawala.
Mkurugenzi wa manispaa anawatafutia ushindi wa
kilazima CCM, ameandika barua ya kupunguza madiwani wa upinzani na kuongeza wa
CCM. Anataka Chadema tuwe na madiwani 12, CUF 6 na CCM 17 ili pawe na tofauti
ya diwani mmoja wakati tulikuwa na tofauti ya madiwani wanne,” amesema Mabina.
Mabina amesema kuwa wakati Mkurugenzi wa Manispaa ya
Kinondoni pia amewaandikia barua ya kuwataka kuwasilisha majina ya madiwani wa
viti maalum upya, hatua ambayo inatafsiriwa kama kutaka kutangaza upya majina
ya wabunge wa viti maalum na manispaa zao, zoezi ambalo lilishafanyika mwaka
jana.
“Mkurugenzi amehamisha wabunge wote wa CCM wa viti
maalum na hata wa kuteuliwa na rais wote wametolewa Ubungo na kupelekwa
Kinondoni akiwemo Dk. Tulia Ackson ambaye anaishi Jimbo la Kibamba.
“Anasahau kuwa kati ya wabunge hao 5 wa CCM, wawili
wa viti maalum na watatu wateule wa rais wamepoteza sifa za kuwa wajumbe wa
Baraza la Manispaa ya Kinondoni kwa kushidwa kuhudhiria kikao chochote tangu
baraza lilipoundwa kwa kumchagua Meya,” amesema Mabina